RUSHWA YA NGONO : Dudu linalofichwa huku likiumiza wengi
“Sote tunakumbuka kwamba, sheria ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya Mwaka 2007, Kifungu cha 25 inafafanua kinaganaga kwa kutofautisha rushwa ya ngono na rushwa nyingine.”
“Kimantiki, sheria hii inakiri kuwa, rushwa ya ngono inatokana na matumizi mabaya ya mamlaka; pale mwenye mamlaka (mwanaume au mwanamke) anapotumia nafasi yake kushawishi, kudai na kulazimisha kutoa haki kwa sharti la ngono.”
Hayo yanasemwa na Mwenyekiti wa Mfuko wa Udhamini wa Wanawake Tanzania (WFT-T), Profesa Ruth Meena katika tamko la pamoja la Wanamtandao wa Kupinga Rushwa ya Ngono Tanzania ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyofanyika Novemba 25 hadi Desemba 10, 2022 iliyokuwa Siku ya Haki za Bidamu Duniani.
Kaulimbiu ya kampeni hiyo kwa mwaka 2022 ilikuwa: “Kila Uhai Una Thamani! Tokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto.”
Katika mzungumzo na HabariLEO, Mkurugenzi Mtendaji wa WFT-T, Mary Rusimbi, anasema: “Kwa kuzingatia kaulimbinu ya kitaifa, Wanamtandao wa Kupinga Rushwa ya Ngono Tanzania wenye mashirika jumuishi zaidi ya 150, tumeamua kuendeleza kampeni ya kitaifa yenye kaulimbiu: “Vunja Ukimya; Rushwa ya Ngono Inadhalilisha na Inaua.”
Rusimbi anakiri kuwa, rushwa ya ngono ni joka hatari lenye maficho mengi akisema: “Rushwa hii haipo tu katika ofisi, bali hata sehemu usizoweza kutegemea kama baadhi ya nyumba za ibada.”
“Ndio maana kutokana na madhara yake, tumekuwa tukifadhili taasisi mbalimbali kama Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) walioamua kuchunguza katika vyuo vikuu na Tamwa (Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania) wakaangalia rushwa katika vyumba vya habari.”
Rusimbi anasema, changamoto kubwa ni kuwa, zipo sehemu ambazo rushwa ya ngono inasemwa zaidi, lakini zipo sehemu nyingine ambazo ipo, lakini hazisemwi jambo ambalo si sawa.
“Lazima ufike wakati sasa jamii iseme hata hapa rushwa ya ngono ipo na hapa ipo na ishirikiane kuvunja mifumo ya ukimya maana tunaponyamaza, tunafanya tatizo liendelee,” alisema.
Anapozungumzia Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katikia Kifungu cha 25, Profesa Meena anasema: “Rushwa ya ngono ni tofauti na rushwa za kawaida zinazohusu mkubaliano ya watu au pande mbili.”
Anasema: “Watetezi wa haki za wanawake na watoto tulisherehekea kwamba hii ni sheria ya kuwalinda wanaoongozwa dhidi ya matumizi mabaya ya mamlaka.”
“Sheria hii imetupa nguvu watetezi wa kupinga vitendo vya rushwa ya ngono kuweka nguvu kubwa kuendesha kampeni ya kuvunja ukimya, kwa kutumia taarifa za kitafiti, kutoka kwa wanahabari na hata matamko ya baadhi ya viongozi ikiwa ni pamoja na viongozi wa dini.”
Mtandao unasema kwa sasa kuna mchakato wa kubadilisha sheria ya kupambana na rushwa ikiwa ni pamoja na Kifungu cha 25 kinachobainisha rushwa ya ngono na rushwa nyingine kwa kuongeza kipengele 25 (ii) kinachofananisha rushwa ya ngono na rushwa nyingine.
Mwenyekiti huyo wa WFT-T anasema: “Sisi wanamtandao tunaopinga rushwa ya ngono tunapinga kitendo cha kuingiza kipengele cha 25 (ii) cha kumhukumu anayedaiwa rushwa ya ngono kwani kufanya hivyo ni kuendelea kuwalinda wenye mamlaka katika ngazi zote kuwanyanyasa, kuwakandamiza na hatimaye kusababisha vifo vya watoto, wanawake na hata vijana wa kiume wa Tanzania.”
Anasema: “Tunaviomba vyombo vyote vinavyohusika na mabadiliko ya sheria hii ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, bunge letu tukufu na hatimaye Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hssam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wasikubali pendekezo la kubadili hiki kifungu pendekezwa cha sheria hii kinachofananisha rushwa ya ngono na rushwa nyingine.”
Kwa mujibu wa mtandao huo, kifungu hicho kinamaanisha kuwa, hata wanafunzi waliofelishwa mitihani kwa kukataa rushwa ya ngono, au wanawake walionyimwa leseni ya biashara kwa kukataa rushwa ya ngono na waathirika wengine, watachukuliwa na sheria kuwa ni wakosaji.
Katika Kongamano la Desemba 13, 2022 katika viwanja vya TGNP Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Taasisi ya Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), Janeth Mawinza, anasema kwa ufadhili wa WFT-T, wameanzisha na kuimarisha klabu za kupinga rushwa ya ngono na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika sehemu mbalimbali mkoani Dar es Salaam.
Anasema, Wajiki inaendesha kampeni ya ‘Safari Salama Bila Rushwa ya Ngono kwa Wasichana na Wanafunzi Inawezeka’ inayolenga kuwajengea uwezo wanaume ili wabadilike na kuwa walinzi wa usalama kwa wasichana na wanawake.
Kampeni hiyo iliyoanza mwaka 2018 mkoani Dar es Salaam na sasa ipo katika awamu ya tano ikifadhiliwa na WFT-T, imewafikia madereva wa bodaboda zaidi ya 6,000 mkoani Dar es Salaam.
Alisema kupitia kampeni hii inayolenga kuchochea vita dhidi ya ukatili wa kijinsia sambamba na rushwa ya ngono kwa wasichana na wanawake hata kupitia vyombo vya usafiri, tayari wamefikia moja kwa moja watu wazima 459, watoto 4,325 wakiwamo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari pamoja na vijana 6,462.
Uchunguzi wa HabariLEO katika vituo mbalimbali vya daladala umebaini kuwa, katika maeneo yenye changamoto za usafiri wanafunzi wa kike wana uhusiano wa kingono na madereva na makondakta wa daladala kiasi cha wasichana hao ‘kumiliki’ daladala.
Makondakta hao huwaachia viti vya mbele wanafunzi wasichana hao wanafunzi hasa nyakati za jioni.
Katika mazungumzo na Gazeti hili, Ismail Abdallah ambaye ni mshiriki katika kampeni hiyo pamoja na Godvoice Kayombo, wanasema wakiwa Vingunguti Ilala kuwa, baada ya kufikiwa na Wajiki na kupata uelewa, wamekuwa mabalozi kwa kuelimisha watu wengine wakiwamo vijana, waendesha bodaboda, bajaji na bodaboda, pamoja na jamii kwa jumla kuhusu madhara ya rushwa ya ngono dhidi ya watoto wasichana hasa wanapokuwa safarini.
“Tunataka daladala, bodaboda na hata bajaji, wawaone wasichana kuwa si tu watoto wa wazazi, bali pia ni watoto wao hivyo wana jukumu la kulinda usalama wao popote walipo,” anasema Kayombo.
Mmoja wa wafanyabiashara ndogo ya vitafunwa katika eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Asha, alisema,rushwa ya ngono inayobeba ubakaji, pia hufanywa na baadhi ya watumishi katika magari ya wanafunzi na waathirika wakubwa ni watoto wanaokuwa wa kwanza kupanda gari na wale wanaukuwa wa mwisho kuteremka.
“Watoto wanaokuwa wa kwanza kuchukuliwa na baadhi ya magari ya shule alfajiri saa 11 na wale wanaokuwa wa mwisho kuteremka, wengine wanafanyiwa ukatili sana; wazazi wawachunguze sana na kwa umakini watoto wao..” alisema Asha.
Mawinza anasisitiza wanaume kutambua na kushiriki juhudi za kumaliza tatizo hili, badala ya kutoa visingizo vinavyolenga kuhalalalisha rushwa ya ngono na ubakaji kwa wasichana na wanawake.
Akizingumzia umuhimu wa jamii kujengewa uwezo zaidi dhidi ya rushwa ya ngono katika kongamano hilo lililofanyika hivi karibuni Dar es Salaam, Mlezi wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Ilala Dar es Salaam, Seleman Bishagazi, anasema elimu zaidi kwa jamii inahitajika.
Anasema wakiwa Singida, mhudumu wa kike katika baa moja alisema: “Hata mteja (mwanaume) animshika maziwa au sehemu yoyote nikiwa kazini nahudumia, hakuna tatizo, shida ni mtu kunifanyia hivyo nje ya mazingira ya kazi…”
“Mkoani Arusha, tulibaini kuwa, mgambo hudai rushwa ya ngono kwa wanawake wafanyabiashara ili wasiwabugudhi wanawake hao wanapofanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa… Kubwa zaidi ambalo ni tatizo, wanawake wengi hawawaambii waume zao changamoto hizi kwa kuwa wanahofia kupata misukosuko ya kutoaminiwa na mume…”
Anasema kwa uchungu: “Kosa kubwa kwa Tanzania na nchi za Afrika Mashariki ni kwamba, hatubebi thamani ya mwanamke na bila kujua, tunazidi kupata hasara… Angalia hata pale Ukonga (Dar es Salaam) watoto wa kike mpaka sasa wanakeketwa. Ni ajabu sana…”
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Womem Innitiatives for Development Organization (TAWIDO) ambayo ni taasisi inayotetea wanawake wasio katika ajira, Sophia Ligalahe, anasema tatizo kubwa linalobainika katika vita dhidi ya ukatili wa kijinsia ni pamoja na ukosefu wa takwimu za litosha na za pamoja.
Akichangia suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Door of Hope Tanzania, Clemence Mwombeki, anasema: “Umefika wakati sasa tujenge mazingira ambapo taarifa za matukio haya zitakuwa na mafanano…”
Naye Mkrugenzi Mkazi wa Global Peae Tanzania, Martha Mghambi, anasema rushwa ya ngono ni tatizo lililosambaa katika sekta nyingi hadi katika mchezo wa mpira wa miguu kwa wanawake.
Kwa upande wake, Ofisa Programu Mwandamizi wa TGNP, Aneth Meena, anasema utafiti wao kwa kushirikiana na WFT-T na Takukuru Mwaka 2020 katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ulibaini kuwa rushwa ya ngono dhidi ya wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine hasa wa kike ni tatizo kubwa.
“Ilibainika kuwa, licha ya kila chuo kuwa na miongozo inayowalinda wanafunzi, uelewa ni mdogo na wenye mamlaka wanatumia mwanya huo kufanya vitendo hivyo viovu…” alisema Aneth.
Akaongeza: “Ilibainika kuwa, wanafunzi wa kiume ambao ni marafiki wa wanafunzi wa kike wanaokataa kutoa rushwa ya ngono kwa wahadhiri, nao huingizwa kwenye matatizo makubwa…”
Anapendekeza: “Kamati za maadili na madawati ya jinsia katika vyuo yatengewe bajeti na kuwezesha wanafunzi kujengewa uwezo ili waweze kutofautisha rushwa ya ngono, ubakaji na biashara ya ngono maana bila fedha yatakuwa madawati jina tu; waelimishwe ajue akiripoti tukio atalindwaje… Vyuo viwekeze katika madawati ya jinsia…”
Kwa mujibu wa Mratibu wa Miradi ya Vijana wa Citizen Fir Change, Raphael Denis, katika kata 18 za Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, wapo wanaume wanaodhani wana mamlaka juu ya maisha ya wanawake na watoto.
“Aidha, wapo wanawake na watoto wanaodhani hawana mamlaka juu ya maisha yao, balo mamlaka hayo yapo kwa wanaume.”