Saba mbaroni wizi fedha za mtandao wa benki

Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Shinyanga, Kenedy Mgani Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Shinyanga, Kenedy Mgani
Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Shinyanga, Kenedy Mgani

KAHAMA, Shinyanga – JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linawashikilia watu saba wakiwemo watumishi watatu wa Benki ya CRDB tawi la Kahama, kwa tuhuma za wizi wa Sh milioni 305 kutoka kwenye akaunti za wateja.

Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Shinyanga, Kenedy Mgani alithibitisha tukio hilo na kwamba watuhumiwa hao wanashikiliwa na polisi.

Alisema tukio hilo ni la juzi saa 8:00 mchana baada ya kuwekewa mtego na jeshi hilo. Alisema watu hao wanne ni kutoka Dar es Salaam majina yao yamehifadhiwa.

Advertisement

Alisema walifika katika benki hiyo kuchukua fedha hiyo katika akaunti za wateja tofauti tofauti wa benki hiyo.

Alisema kupitia mtego huo watu hao waliingia katika benki hiyo na kwenda kwa meneja huduma kwa wateja wa benki aliyewasikiliza na kuwaagiza watumishi wengine wawili wawahudumie.

SOMA: Serikali yasitisha uchenjuaji dhahabu mgodi EMJ Simiyu

Alisema walipoanza kuwahudumia walitoa Sh milioni 30 kwa kutumia kadi bandia kwa moja ya akaunti ya wateja. “Na baadaye walitoa shilingi milioni 275 ndipo walipokamatwa kutokana na mtego uliokuwa umewekwa na polisi na benki hiyo,” alisema Mgani.

Alisema watu hao wamekuwa wakijishughulisha na wizi kwenye mitandao na jeshi linaendelea kuwatafuta wengine. Mgani alitoa wito kwa wateja wa benki kuwa na tabia ya kukagua mitandao yao na taarifa za fedha zao kwenye akaunti zao kudhibiti matapeli na wezi wa mtandaoni.