Samia aiagiza tena Polisi ajali za barabarani

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka madereva wa vyombo vya usafiri kuendelea kuwa makini na waangalifu zaidi barabarani na kuliagiza Jeshi la Polisi kuendelea kusimamia sheria za usalama barabarani wakati huu wa mwisho wa mwaka.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya kuripotiwa kuwa vifo vya watu 10 waliokufa kwenye ajali iliyotokea Desemba 26, mwaka huu saa 9:40 alasiri katika Kijiji cha Kibaoni, Tarafa ya Tarakea wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.

Hadi sasa inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 50 wamefariki kutokana na ajali za barabarani kuanzia Desemba Mosi hadi Desemba 26, mwaka huu.

Advertisement

Ajali ya Rombo imehusisha magari mawili ya abiria; Toyota Noah lenye namba za usajili T 959 CKU lililotokea Tarakea kwenda Moshi na lingine ni la Kampuni ya Ngasere lenye namba za usajili T 620 DZQ likitokea Dodoma kwenda Tarakea.

“Nimesikitishwa na taarifa ya vifo vya ndugu zetu tisa kutokana na ajali ya barabarani iliyotokea katika barabara ya kutoka Tarakea, Wilaya ya Rombo kuelekea Mji wa Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro,’’ ameandika Rais Samia.

Pia aliongeza: “Nawaombea marehemu wapumzike kwa amani. Ninatoa salamu za pole kwa wafiwa, ndugu na jamaa, na ninawaombea majeruhi wapate nafuu kwa haraka.

“Nasisitiza madereva kuendelea kuwa makini na waangalifu zaidi barabarani, huku Jeshi la Polisi likiendelea na kazi ya kusimamia sheria za usalama barabarani wakati huu wa mwisho wa mwaka”.

Hivi karibuni, Rais Samia aliagiza Jeshi la Polisi kuwa na mfumo wa leseni za udereva utakaoweza kuwapunguzia alama (pointi) madereva wanaofanya makosa yenye kuhatarisha usalama na uhai barabarani.

“Mfumo huu uweke taarifa (kumbukumbu) kielektroniki za mwenendo wa makosa ya madereva barabarani kitakwimu, na kisha utumike kuamua kama wanastahili kuendelea kuwa na leseni za udereva au la. Hii ni katika kuboresha mfumo wa sasa ambao mara nyingi dereva hulipa faini pekee na kuachwa kuendelea kuwepo barabarani,” aliagiza Rais Samia hivi karibuni.

Mbali na ajali hiyo, usiku wa mkesha wa Krismasi, watu 11 walifariki dunia na wengine 13 walijeruhiwa katika ajali iliyohusisha lori na basi dogo la abiria eneo la Kwankwale, Kata ya Kitumbi wilayani Handeni mkoani Tanga saa 3:00 usiku.

Ajali hiyo ilihusisha basi dogo la abiria aina ya Nissan Civilian lenye namba T 497 DZW lililokuwa linatoka Mkata kwenda Tanga Mjini na lori aina ya Fuso lenye namba T 707 EBZ lililokuwa linatoka Lushoto kwenda Dar es Salaam.

Tanzania inatakiwa kutekeleza Azimio la Umoja wa Mataifa la Muongo wa Utekelezaji wa Usalama Barabarani 2022-2030 la kupunguza vifo na majeruhi watokanao na ajali za barabarani kwa angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani, vyanzo vikuu vya ajali za barabarani ni sababu za kibinadamu zinazotokana na uzembe, mwendokasi, uendeshaji wa hatari, kupita gari bila uangalifu unaochangia kwa asilimia 93.90 wakati ubovu wa vyombo vya usafiri ni asilimia 4.1 na sababu za kimazingira, ikiwamo miundombinu mibovu ya barabara ni asilimia 2.0.

Ripoti ya Hali ya Usalama Barabarani iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuanzia Januari hadi Desemba 2023, ilionesha kuwa matukio ya ajali yaliongezeka kwa asilimia 0.8 ambako matukio 1,733 yaliripotiwa nchi nzima ikilinganishwa na matukio 1,720 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.

Katika matukio hayo, ajali 1,118 zilisababisha vifo ikilinganishwa na matukio ya ajali 1,064 zilizoripotiwa mwaka 2022, ikiwa ni ongezeko la matukio ya ajali 54 sawa na asilimia 5.1.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu 1,647 walifariki dunia katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka 2023 ikilinganishwa na watu 1,545 waliofariki mwaka 2022 na kufanya ongezeko la vifo vya watu 102 sawa na asilimia 6.6.

Aidha, watu 2,716 walijeruhiwa ikilinganishwa na majeruhi 2,278 waliojeruhiwa mwaka 2022 sawa na ongezeko la majeruhi 438 ambao ni sawa na asilimia 19.2.

Juni mwaka huu, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, alisema katika kipindi cha miaka mitano kutoka mwaka 2019 hadi Mei 2024, ajali za barabarani zilikuwa 10,093, vifo vilikuwa 7,639 na majeruhi 12,663 miongoni mwao wakipata ulemavu wa kudumu.

Kati ya ajali hizo, magari binafsi yalisababisha ajali 3,250, vifo 2,090 na majeruhi 3,177 wakati magari ya kukodi kwa ajili ya sherehe, misiba na shughuli maalumu yalisababisha ajali 326, vifo 263 na majeruhi 302.

Kadhalika, mabasi ya abiria yalisababisha ajali 790, vifo 782 na majeruhi 2,508 huku daladala zikisababisha ajali 820, vifo 777 na majeruhi 1,810 na taksi zikichangia ajali 93, vifo 97 na majeruhi 173.