BARAZA la Umoja wa Afrika limepitisha Azimio la Dar es Salaam kuhusu nishati safi ya kupikia.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga imeeleza kuwa baraza hilo limemtambua na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kama kinara wa ajenda hiyo Barani Afrika.
Nyanga alieleza kuwa awali rais alishiriki katika kikao cha pembezoni cha Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSSCC).
Aliwashukuru wakuu hao wa nchi kwa kushiriki kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu Nishati wa Misheni 300, uliofanyika Dar es Salaam.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CAHOSSC Rais wa Kenya, William Ruto, Rais Samia aliwasilisha Azimio la Dar es Salaam.
Alieleza kuwa Afrika inapaswa kuendelea kushiriki kikamilifu kwenye majadiliano ya mabadiliko ya tabianchi, kutetea maslahi ya Afrika na kuhakikisha inakuwa na mbinu mpya za kutetea na kutumia rasilimali zake katika kukabili mabadiliko ya tabianchi.
Rais Ruto alimpongeza Rais Samia kwa kufanikisha mkutano wa Misheni 300, na kikao kiliridhia Azimio hilo kuwasilishwa kwenye Baraza la Umoja wa Afrika kwa ajili ya kupitishwa na baraza hilo.
Nyanga alieleza kuwa baraza lilipitisha Azimio hilo bila kupingwa.
Rais Samia pia aliwasilisha ajenda ya nishati safi ya kupikia iliyopendekezwa na Tanzania katika Baraza la Umoja wa Afrika.
Alieleza kuwa nishati safi ya kupikia ni hitaji muhimu kwa watu milioni 900 barani Afrika wasiotumia nishati hiyo kwa sasa.
Awali, juzi Mkutano wa Kawaida wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliichagua Tanzania kuwa mjumbe wa Kamati ya Uongozi wa Umoja wa Afrika kwa mwaka 2025.
Kamati hiyo inaundwa na Angola kutoka Kanda ya Kusini (Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika 2025), Burundi kutoka Kanda ya Kati (Makamu wa Kwanza wa Mwenyekiti), Ghana kutoka Kanda ya Magharibi (Makamu wa Pili wa Mwenyekiti) na Tanzania kutoka Kanda ya Mashariki (Makamu wa Tatu wa Mwenyekiti).
Aidha, Mauritania iliyokuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kwa mwaka 2024 kutoka Kanda ya Kaskazini itakuwa Katibu wa kamati hiyo.