Samia apigania ajira na nishati safi EAC

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesisitiza juu ya umuhimu wa juhudi za pamoja katika kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia na ajira kwa vijana ili kuhakikisha ustawi wa watu wa kanda hiyo.

Rais Samia amesema hayo Arusha wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yaliyofanyika jijini Arusha.

Amesisitiza umuhimu wa kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kanda hiyo kupunguza athari za
kimazingira na kuwaepusha wanawake na matatizo ya afya ya kupumua.

Advertisement

Amesema serikali yake itaendelea kusimamia matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza vifo vinavyotokana na utoaji wa hewa ya kaboni kutoka kwenye mkaa na kuni.

SOMA: Mwenyekiti EAC kupatikana Novemba 30

Amesema Tanzania imejiwekea lengo la kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, angalau asilimia 80 ya Watanzania  watumie nishati safi ya kupikia.

“Katika juhudi zetu za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, tumeamua kwamba kila wilaya
itapanda miti 1.5 kila mwaka, huku tukiwekeza kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesema Samia.

Ameongeza: “Tanzania ina vijiji 12,300, hivyo tunachofanya ni kuunganisha vijiji vyote hivi umeme kusaidia watu
wetu kujihusisha na masuala ya biashara hasa wanawake na vijana”.

Amesema Tanzania inawekeza katika uzalishaji wa umeme, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha zaidi ya MW 2,000.

Alifafanua Tanzania ipo katika mchakato wa kuzalisha nishati mbadala kupitia nishati ya jua na upepo na kujua
namna ya kutumia mabaki ya mkaa kutengeneza gesi safi ya kupikia.

Rais Samia amesema juhudi hizo ni sehemu ya kupambana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi, kwani Tanzania inapoteza takribani ekari 400,000 za ardhi kila mwaka.

Amesema kutokana na halo, Tanzania inatumia kati ya asilimia nne hadi tano ya pato lake la taifa kupambana na uharibifu wa mazingira.

Ili kufanikisha matumizi ya nishati safi kwa wanawake na wanaume, aliwahimiza viongozi wa EAC kuungana
kuendeleza ajenda hiyo kwa manufaa ya watu wao.

Naye, Rais Yoweri Museveni wa Uganda amezikumbusha nchi za EAC kuhusu maono ya waasisi wake kama Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Jomo Kenyatta na Rais Milton Obote, ambao walikusudia kuunda ushirikiano utakaokuza ustawi wa watu na usalama.

Rais William Ruto wa Kenya amesisitiza nchi yake itajitolea katika kuimarisha amani na usalama katika EAC
ili wananchi waweze kufanya biashara kwa amani.

Naye, Rais Hassan Mahmoud wa Somalia ameishukuru EAC kwa kuikaribisha nchi yake kwenye jumuiya, akisema
hatua hiyo itasaidia kuimarisha uchumi wa nchi hiyo.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Burundi, Prosper Bazombaza amesisitiza umuhimu wa kuboresha biashara za mipakani kwa kushughulikia vikwazo vya biashara (NTBs).