Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kusimamia malengo ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya kujenga ustawi wa wananchi ikiwemo kwa kuboresha sekta ya elimu.
Akizungumzia dhana pana ya Mapinduzi, Rais Dk Samia amesema “Mapinduzi ni maendeleo, hatua baada ya hatua. Yale Mapinduzi ya kuutafuta Uhuru tulimaliza, sasa hivi ni Mapinduzi ya kutafuta maendeleo, hatua baada ya hatua, na kulinda Uhuru wetu; ndio Mapinduzi yetu sasa hivi”.
Aameyasema hayo leo wakati akizindua Skuli ya Sekondari Bumbwini Misufini, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha, kutokana na mchango mkubwa wa Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Rais Dk Samia ameelekeza skuli hiyo ibebe jina la kiongozi huyo kwa heshima yake.
SOMA: “Miaka 61 ya Mapinduzi nchi ina maendeleo makubwa”
Asesema skuli hiyo ni matokeo ya maono ya Viongozi wa Mapinduzi waliodhamiria fursa ya elimu itolewe kwa watu wote, jambo ambalo limeendelea kusimamiwa na Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi.
Rais Dk Samia ameongeza kuwa hatua kubwa imepigwa katika sekta ya elimu huku idadi ya skuli pamoja na wanafunzi kuanzia elimu ya awali hadi sekondari ikiongezeka ikiwa ni matunda na matokeo ya Mapinduzi.
Amesisitiza kuwa shabaha ya Serikali zote mbili ni kujenga mfumo wa elimu unaozalisha wanafunzi wenye utaalamu na ujuzi, utakaowawezesha kushindana katika soko la ajira na kulinufaisha Taifa kwa ujumla.
Akizungumzia umuhimu wa masomo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), amesema kuwa Serikali inatekeleza Mkakati wa Uchumi wa Kidigitali ili kuwaandaa Watanzania kunufaika na ajira zinazozalishwa kupitia uwekezaji unaofanywa nchini ikiwemo kuziwezesha shule/skuli kuwa na mifumo ya TEHAMA.
Kwa upande mwingine, Rais Dk Samia ametoa rai kwa wazazi kuwapa watoto wao nafasi ya kupata fursa ya elimu, ikiwemo kuwapatia muda wa kupitia masomo yao na kwenda shule/skuli wakiwa katika hali inayotakiwa.