Samia atoa mil 50/ kuwezesha wanawake wa Samia

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu ametoa kiasi cha Sh milioni 50 kwa Taasisi ya Wanawake na Samia Mkoa wa Geita ili kuwawezesha kupanua uwigo wa uwekezaji wa mradi wa chakula na mkaa mbadala.

Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya Rais Samia kutembelea banda la Wanawake na Samia kabla ya kufunga Maonyesho ya Saba ya Teknolojia ya madini ambapo alivutiwa na shughuli za kikundi hicho.

Advertisement

Akikabidhi hundi ya pesa hiyo ofisini kwake mjini Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine amesema pesa hiyo ni hamasa ya kuwezesha taasisi hiyo kupiga hatua zaidi na kuwainua wanawake kiuchumi.

“Matarajio yetu ni kwamba milioni 50 ambayo imetolewa, ni chachu ya kuongeza mtaji waliokuwa nao, lakini chachu ya kufanya biashara ya Wanawake na Samia itengeneze faida.

SOMA: Rais Samia atoa agizo la wanawake

“Mtaji huu utaenda kuongeza mtaji uliokuwepo kwenye Wanawake na Samia na kuwezesha taasisi ya Wanawake na Samia kuanza kushindana kwenye fursa zingine za kibiashara,” amesema Shigella.

Ameongeza, serikali inatarajia kuona Wanawake na Samia wanakuwa wazalishaji wakubwa wa mkaa mbadala ili kuunga mkono matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Hii siyo pesa ya kwenda kugawana posho, pesa hii imeletwa kuinua mitaji, mtaji utengeneze faida, faida itakayopatikana ndiyo itaenda kuiwezesha taasisi ya Wanawake na Samia kiwilaya na kimkoa,” amesisitiza.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Samia Mkoa wa Geita, Adelina Kabakama amesema pesa hiyo itawasaidia kukua zaidi kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya hadi kata ili kufikisha malengo ya taasisi.

SOMA:  Rais Samia atoa agizo la wanawake

Amesisitiza kuwa pesa hiyo inaenda kuongeza uwekzaji wa taasisi kwenye maeneo yao mawili ambayo ni biashara ya chakula na uzalishaji wa mkaa mbadala.

Mwenyekiti wa Kupinga Ukatili katika taasisi ya Wanawake na Samia, Nuru Kijazi amesema baada ya kupata tenda ya kulisha watumishi wa Stamico ndani ya GGML walikuwa hawana mtaji wa kutosha.

“Kwa sasa hivi hatutapata tena ile changamoto ya kukopa pesa kwa ajili ya kuweza kutimiza kupika chakula kwa ajili ya hiyo tenda tuliyopewa na Stamico,” amesema Nuru.