Samia: CCM inaaminika

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan amesema CCM inatimiza miaka 48 ikiwa imara, chama kikubwa na kinachotumainiwa zaidi ndani na nje ya Tanzania.

Amesisitiza pia, kwamba CCM haitobadili itikadi yake katika kuwatumikia wananchi kwa kuwa binadamu wote ni sawa, hivyo wanastahili kupata maendeleo.

Rais Samia amesema hayo alipozungumza na wana CCM wakati wa maadhimisho ya miaka 48 ya chama hicho yaliyofanyika jijini Dodoma.

Advertisement

Amesema kuwa CCM ni chama kinachowaunganisha watu na kuhubiri umoja kwani chimbuko lake ni umoja.

“CCM imeendelea kubaki katika msingi wa umoja, kuwa nguzo imara katika kudumisha amani na mshikamano wa
taifa, msingi huo wa umoja ndio umefanya CCM imeendelea kuheshimiwa, kuthaminiwa na kutumainiwa ndani na nje ya Tanzania na kuaminiwa na wananchi na kupewa fursa ya kuaminiwa kuongoza serikali zote mbili,” amesema Rais Samia.

Ameongeza: “Tunapoadhimisha miaka 48, niahidi kuwa CCM haitabadili itikadi yake ya kuwatumikia watu wake na imani yake kwamba binadamu wote ni ndugu zetu na Afrika ni moja”.

Rais Samia amesema kuaminika kwa CCM ni matokeo ya jitihada za kushughulikia matatizo ya wananchi kupitia utekelezaji ahadi zake kupitia Ilani ya Uchaguzi.

Amesema CCM itaendelea kutekeleza wajibu wake katika kuwaletea wananchi maendeleo kupitia serikali zote mbili.

Rais Samia amesema kutokana na utekelezaji wa Ilani anaamini uchaguzi wa mwaka huu hautakuwa tofauti kwa kuwa Watanzania wataendelea kuipa CCM dhamana ya kuendesha serikali zote mbili.

“Pamoja na hali hiyo tusibweteke, ndugu zangu pamoja na hali hiyo ya kujiamini kwamba CCM ni chama kikubwa na tunamatumaini makubwa kwenye uchaguzi ujao, tusibweteke,” amesema.

Ameongeza: “Tunapoadhimisha miaka 48 ya chama chetu, tuwahakikishie wananchi kuwa CCM imejipanga kuendelea kutoa uongozi thabiti kwa ustawi wa taifa letu”.

Amesema mwelekeo wa CCM kwa miaka mingi ijayo itategemea kasi ya chama katika kubaini changamoto mpya na
kunyumbulika kwa wakati katika kuzitatua na kutolea mfano changamoto ya ajira ambayo chama hicho kimeibaini.

Rais Samia amesema CCM ina mtaji mkubwa kutokana na kukubalika kwake kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani yake.

“Pia, tuna wingi wa wanachama, kwa sasa CCM ina zaidi ya wanachama milioni 12, wapenzi wengi sana na pia, ni upana wa mtandao wetu unaotokana na jumuiya zetu na umadhubuti wake,” amesema.

Rais Samia amesema CCM itaendelea kujiimarisha zaidi ndani ya chama na akaagiza viongozi wawafikie wananchi kuwasikiliza na kutatua changamoto zao na kuongeza matumizi ya Tehama ili kukuza na kurahisisha mawasiliano.

Amewahakikishia wana CCM kuwa chama kitahakikisha haki inatendekea katika kupata wagombea wanaotokana na nacho.

“CCM tutawaletea wagombea wanaokubalika ili kuwapa wananchi wepesi wa kuweka mafiga matatu yaani Rais,
wabunge na madiwani,” amesema Rais Samia.

Amesema CCM imejipanga kuendelea kutoa uongozi thabiti kwa manufaa ya nchi kwani demografia ya nchi na mabadiliko ya teknolojia yanaonesha kukubalika kwa CCM na hatima ya kesho yake, inategemea kile kinachokifanya leo.

Rais Samia amesema ni muhimu kujipanga kwa kujipima kwa sera, mipango na kazi nzuri ambazo serikali inazifanya na namna zinavyoleta matokeo kwa wananchi.

Amesema CCM imebaini changamoto kubwa inayoikabili dunia ni tatizo la ajira kwa vijana, hivyo serikali imeanza kwa kufanya mabadiliko ya sera ya elimu na mafunzo.

Rais Samia amesema mabadiliko hayo yamelenga kuwafanya wanafunzi wapate elimu itakayowapa ujuzi watakaoutumia kujiingizia kipato kupitia fursa zilizopo.

Amesema pia, hatua nyingine iliyochukuliwa katika kukabiliana na hali hiyo ni kuvutia fursa za uwekezaji katika sekta ya michezo, utalii na kuibua programu za kuwajengea uwezo vijana.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *