SHIRIKA Lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na utoaji wa msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto (NERIO) katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara limetambulisha rasmi mradi wa Sauti ya Mwanamke kwa wadau mbalimbali kwenye manispaa hiyo.
Akizungumzwa wakati wa ghafla fupi ya kutambulisha mradi huo kwa wadau wa manispaa hiyo, Mratibu wa Shirika hilo, Saidi Ismail amesema mradi una lenga kumwinua mwanamke, mtoto wa kike pamoja na watu wenye mahitaji maalumu.
Amesema miongoni mwa majukumu ya mradi kwa makundi hayo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha yanapata haki zao kwa mujibu wa sheria ikiwemo kutambua wajibu wao, haki zao lakini sehemu sahihi ya kwenda kuwasilisha changamoto zao hasa wanapohitaji kupata msaada wa kisheria.
Soma Zaid: https://habarileo.co.tz/dc-mbogwe-awataka-wanawake-kushiriki-maendeleo/
Utambulisho wa mradi huo umefanyika katika manispaa hiyo na unatekelezwa kwenye kata 8 zilizopo kwenye manispaa kwa kipindi cha miezi kumi na moja kuanzia Januari 2025 mpaka Novemba mwaka huu.
Ofisa Mradi wa shirika hilo, Judith Chitanda amesema lengo la mradi ni kufikia jamii yenye usawa hasa wanawake na utawafikia watu zaidi ya 13,000 elfu huku ukigharimu Sh milioni 28.
“Tutatoa elimu kwa jamii kuhusiana na masuala mbalimbali ya sheria hasa masuala ya ardhi, miradhi, ndoa na matunzo ya watoto, kama tunavyojua wanawake wengi ni wahanga wa vitendo vya ukatili ya kijinsia na ni janga la kitaifa na manispaa yetu ni miongoni mwa wanawake wengi waliyofanyiwa vitendo hivi,”amesema Chitanda.
Soma zaidi: https://habarileo.co.tz/tngp-yawataka-wanawake-kushiriki-uchaguzi-mitaa/
Mkurugenzi wa Mtandao wa Mshirika yasiyo ya Kiserikali (MTWANGONET) mkoani humo, Fidea Luanda amesema ni imani yake kuwa mradi huo utaenda kutatua tatizo lililopo kwenye jamii yao kwa pale watakapoanzia utekelezaji hatimaye kuleta mabadiliko na kama wadau watahakikisha wanaunga mkono jitihada hizo.
Diwani wa Kata ya Chikongola, Mussa Namtema amesema: “Nawapongeza shirika la Nerio kwa kupata mradi huu unaotekelezwa kwenye manispaa yetu, kikubwa niwaombe wananchi wetu waupokee vizuri mradi ili uweze kusaidia kutatua matatizo yao mbalimbali ya kisheria.’’