Sekta isiyo rasmi na mchango kiuchumi usiotambulika

Biashara ya chakula ni huduma muhimu kwa jamii.

SEKTA isiyo rasmi Tanzania ndiyo nguzo ya uchumi wa taifa kwa kuwa inategemewa na mamilioni ya Watanzania kama njia muhimu na salama ya wasio na ajira rasmi kujipatia riziki huku ikifanya shughuli za kiuchumi nje ya udhibiti na ulinzi wa serikali.

Inajumuisha biashara ndogondogo ambazo hazijasajiliwa, wachuuzi wa mitaani (wamachinga) na waendesha pikipiki za biashara (bodaboda), wakulima na wachimbaji wadogo.

Sekta hii ni nguzo imara ya uchumi wa nchi kwa kuwa inachangia ajira kwa kiasi kikubwa, inasaidia kupunguza
umasikini na pia ina mchango mkubwa katika pato la taifa.

Advertisement

Umuhimu wa sekta isiyo rasmi
Sekta isiyo rasmi nchini si tu kwamba ni shughuli ya kiuchumi, bali pia ni nguzo kuu ya uchumi wa nchi. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO), nchini Tanzania sekta isiyo rasmi huchangia zaidi ya asilimia 50 ya pato la taifa na kuajiri zaidi ya asilimia 80 ya wafanyakazi.

Hili linajidhihirisha wazi katika maeneo ya mijini kama Dar es Salaam, Mwanza na Arusha. Katika miji kama hii,
biashara na huduma zisizo rasmi huchukua nafasi kubwa kiuchumi. Katika maeneo ya vijijini, shughuli zisizo rasmi kama kilimo kidogo na uchimbaji madini ndizo vyanzo muhimu vya mapato ya kaya mbalimbali.

Wakulima wadogo vijijini huchangia uendelevu wa kaya na huduma kwa jamii.

Mmoja wa wachumi aishiye Mwanza, Dk Jane Mtei anasema, “Sekta isiyo rasmi ni uti wa mgongo wa uchumi wa
Tanzania. Ndiyo inachukua nguvukazi kubwa hasa vijana na wanawake ambao mara nyingi hukosa fursa za ajira
rasmi.”

Mfanyabiashara mdogo katika Barabara ya Makongoro jijini Mwanza, John Mwakatobe, anaunga mkono kauli hii akisema, “Bila sekta isiyo rasmi, wengi tusingeweza kuhudumia familia zetu. Sekta hii si tu kwamba ni kazi, bali ni
njia ya maisha.”

Umuhimu wa sekta isiyo rasmi nchini unadhihirishwa zaidi katika nafasi yake kupunguza umasikini. Shughuli zisizo  rasmi ndizo chanzo kikuu cha mapato kwa Watanzania wengi hasa wa vijijini.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya 2021, nchini Tanzania asilimia 76 ya kaya zinazoishi vijijini hutegemea shughuli za sekta isiyo rasmi kwa kipato na maisha yao. Umuhimu huu unadhihirika zaidi katika mikoa kama Dodoma na Singida ambako shughuli za kilimo na biashara ya mifugo ndizo tegemeo kuu la uchumi wa ndani.

Sifa za sekta isiyo rasmi
Sekta isiyo rasmi nchini ipo katika namna mbalimbali ikijumuisha shughuli kadhaa. Pamoja na mambo mengine
mengi, sekta hii inahusisha biashara ndogondogo (uchuuzi/ umachinga) mitaani, uzalishaji katika viwanda vidogo, bodaboda na uchimbaji madini usio rasmi.

Kilimo kisicho rasmi na biashara ya mifugo ni shughuli zilizoenea zaidi vijijini. Sifa kubwa ya sekta hii ni kupokea mabadiliko na kuruhusu watu binafsi kuzalisha mapato kwa kutumia mtaji mdogo na miundombinu iliyopo.
Kidemografia, sekta inaongozwa na vijana na wanawake.

Kwa mujibu wa Ripoti ya NBS ya Mwaka 2022, nchini Tanzania asilimia 65 ya wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi wana umri wa chini ya miaka 35 na wanawake ni karibu asilimia 60 ya nguvukazi. Hata hivyo, mara nyingi
wafanyakazi hawa wanakabiliwa na hali ngumu ikiwamo ya mishahara/ujira duni, ukosefu wa ulinzi wa kijamii na upatikanaji duni wa huduma za kifedha.

Katika maeneo ya mijini kama vile Dar es Salaam, sekta isiyo rasmi inaonekana sana kwa wamachinga wanaojipanga katika barabara na masoko wakiwa na shughuli mbalimbali. Kwa mfano, Mama Nuru wa Katesh mkoani Manyara
(45) ni mchuuzi wa mtaani ambaye amekuwa akiuza matunda na mboga kwa zaidi ya miaka 15.

Licha ya kufanya kazi kwa bidii, anapata ugumu kupata mikopo kuendeleza biashara yake. Anasema, “Nilijaribu kuomba mkopo benki, wakaniomba hati ambazo sina.” Yaliyomkumba, Mama Nuru ni kawaida kwa wamachinga wengi nchini kote ambao mara nyingi hukosa dhamana na nyaraka zinazohitajika na taasisi rasmi za kifedha, zikiwamo benki ili kupata mkopo.

Katika maeneo ya vijijini, shughuli zisizo rasmi zinaweza kuwa hazionekani sana, lakini si kwamba zina umuhimu
mdogo. Mkoani Geita kwa mfano, uchimbaji dhahabu usio rasmi husaidia na kuendeleza maisha ya maelfu ya watu na unachukua nafasi muhimu katika uchumi wa ndani.

Mfanyabiashara mdogo wa Geita, Juma Ali (30) anaelezea uhalisia kuhusu ugumu katika kazi yake. Anasema, “Tunafanya kazi kwa saa nyingi, lakini mapato hayatabiriki na mara nyingi hayatoshi kujikimu.” Mfano huu unaakisi ugumu wanaokumbana nao watu wengi wanaotegemea uchimbaji madini usio rasmi kama chanzo chao cha mapato.

Makamu Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania, Victor Tesha anasisitiza umuhimu wa sekta isiyo rasmi akisema, “Kwa wengi, uchimbaji madini usio rasmi si tu kazi, bali njia ya kuokoa maisha. Licha ya hayo, juhudi za kuifanya sekta isiyo rasmi kuwa rasmi (kurasimisha) zinakabiliwa na vikwazo kadhaa zikiwamo gharama kubwa za urasimishaji na urasimu.

Uwepo wa huduma za bodaboda mijini na vijijini umerahisisha usafiri kwani hupatikana kirahisi, haraka na kufika hadi mitaani.

Kama ilivyo kwa Juma, wachimbaji madini wengi wanaangukia kutokuwa rasmi jambo ambalo ni hatari kubwa na njia chache mbadala. Sera na changamoto zilizopo Serikali ya Tanzania inafanya juhudi kubwa kudhibiti na kusaidia sekta isiyo rasmi kupitia sera, sheria na programu mbalimbali.

Mmoja wa wabunge mkoani Dodoma (jina linahifadhiwa) anasema, “Sera ya Taifa ya Ajira Tanzania inalenga kuifanya mabadiliko sekta hii kwa kuweka mazingira wezeshi kwa biashara zisizo rasmi kujiendesha, kuboresha tija na kurasimisha taratibu. “Hii inahusisha kupata mafunzo, miundombinu, masoko pamoja na mipango mingine
kama vile kurahisisha kanuni, kutoa vitambulisho kwa wamachinga na kusaidia vyama katika sekta isiyo rasmi.”

Sheria muhimu, ikiwamo Sheria ya Fedha ya 2020 zinarahisisha usajili wa kodi kwa biashara ndogo na kurahisisha mpito kwa uchumi rasmi huku Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya 2004 ikitoa mfumo wa kulinda haki za wafanyakazi, ingawa bado utekelezaji wake ni changamoto.

Programu kama vile Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) hutoa masharti katika uhamishaji wa fedha na mafunzo ya ujuzi kwa kaya zilizo katika mazingira magumu zinazotegemea shughuli zisizo rasmi.

Taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) kama vile Foundation for Civil Society (FCS) pia, huchangia kwa kutoa elimu ya fedha na mafunzo ya ujasiriamali ili kuwawezesha wafanyakazi wasio rasmi. Hata hivyo, bado kuna changamoto kwa kuwa biashara nyingi zisizo rasmi zinapata ugumu kupata huduma rasmi za kifedha kwa kukosa dhamana au historia ya mkopo.

Urasimu na kodi kubwa pia, hukatisha tamaa na kukwamisha urasimishaji wa shughuli nyingi za sekta isiyo rasmi.
Mtaalamu wa maendeleo aliyeko Zanzibar, Dk Fatma Suleiman anasema, “Pengo kati ya sera na utekelezaji ni kubwa.”

Anasema ugumu wa kuelewa mifumo ilivyo au kujua haki zinazopatikana hupunguza upatikanaji wa msaada. Moja ya changamoto kuu ni ukosefu wa mbinu pekee kusaidia sekta isiyo rasmi huku kukiwa na sera na programu nyingi ambazo mara nyingi hugawanyika na kukosa uratibu sahihi.

Hali hii imefanya wafanyakazi wengi wasio rasmi, kuachwa bila msaada wanaohitaji kukuza biashara zao na hata kuboresha maisha yao.

Mzigo, changamoto za kiuchumi
Mchango wa sekta isiyo rasmi katika uchumi wa Tanzania hauwezi kupuuzwa kwa kuwa ni kichocheo kikuu cha ajira hasa katika maeneo ya mijini ambapo nafasi rasmi za kazi ni chache.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, biashara zisizo rasmi huchangia zaidi ya asilimia 70 ya ajira zisizo za kilimo nchini.
Sekta hii pia, ni muhimu katika maendeleo mijini na vijijini ikitoa bidhaa na huduma za bei nafuu ambazo watu wengi humudu na kusaidia minyororo ya usambazaji wa ndani.

Katika maeneo ya vijijini, shughuli zisizo rasmi kama kilimo kidogo na uchimbaji madini ni muhimu kwa mapato ya kaya na uchumi wa ndani. Mfano ni eneo la Ziwa Victoria Goldfield linalozunguka mikoa kama Mwanza, Geita,
Mara na sehemu za Shinyanga.

Katika eneo hili, uchimbaji usio rasmi wa dhahabu huajiri maelfu ya watu binafsi na kuwa chanzo muhimu cha
mapato kwa familia na kuchochea shughuli za kiuchumi katika jamii hizi. Hata hivyo, mara nyingi shughuli hizi huja na gharama kubwa.

Wachimbaji na wakulima kwa kawaida hufanya kazi katika hali hatarishi huku wakiwa hawana vifaa vya usalama, kinga za kisheria wala mifumo rasmi ya msaada. Kwa mfano, wachimba madini wa Mara na Geita mara nyingi hukumbwa na matukio ya hatari kama kuporomokewa na udongo wakiwa shimoni, kuathiriwa na kemikali zenye
sumu na athari za muda mrefu za kiafya huku wakipata mapato yasiyotabirika.

Kadhalika, wakulima wadogo wa mikoa ya Shinyanga na Mwanza hukabiliana na changamoto kadhaa zikiwamo za upatikanaji mdogo wa masoko, miundombinu duni na ukosefu wa uhakika wa hali ya hewa.

Hata hivyo licha ya magumu hayo, ustahimilivu wa watu wanaojishughulisha na shughuli zisizo rasmi unadhihirisha umuhimu wao kwa maisha ya vijijini.

Michango yao si tu kwamba inadumisha, bali pia huendesha uchumi wa ndani katika maeneo husika hivyo kubainisha hitaji la lazima la sera zinazoshughulikia upungufu uliopo huku zikilinda nafasi yao muhimu katika muundo wa uchumi nchini.

Sekta isiyo rasmi pia, ina nafasi muhimu katika maendeleo ya miji. Katika miji kama Dar es Salaam na Mwanza,
biashara zisizo rasmi ndizo hutoa bidhaa na huduma muhimu kwa jamii zenye kipato cha chini. Kuanzia kwa wachuuzi wa chakula (mama/babalishe) hadi bodaboda, shughuli hizi huziba pengo linaloachwa na sekta rasmi na kuhakikisha hata kaya masikini zaidi zinapata mahitaji.

Mwendesha bodaboda wa jijini Mwanza, Rajab Simba (28) anasema kila siku hukabiliwa na changamoto kadhaa,
zikiwamo za kunyanyaswa na mamlaka za mitaa na ukosefu wa vifaa vya usalama. “Tunatoa huduma muhimu
kwa jamii, lakini mara nyingi tunachukuliwa kama wahalifu,” anasema Simba.

Uzoefu wa Rajab unadhihirisha hitaji la udhibiti borana msaada kwa watoa huduma hizo za usafiri wasio rasmi.

Changamoto za kisekta
Hata hivyo licha ya umuhimu wake, sekta isiyo rasmi inakabiliwa na changamoto nyingi. Upatikanaji wa fedha ni kikwazo kikubwa. Biashara nyingi zisizo rasmi haziwezi kupata mikopo kutoka katika taasisi rasmi na hii
inachangiwa pia, na vikwazo vya kisheria na vya kiudhibiti.

Kwa mfano, mchakato wa kurasimisha biashara nchini unaweza kuwa wa gharama kubwa na unaochukua muda
mrefu, hali inayowakatisha tamaa wafanyabiashara wengi. Upungufu wa miundombinu pia, huongeza changamoto hizi.

Mitandao mibovu ya barabara, ukosefu wa masoko na mafunzo hukwamisha ukuaji na tija ya biashara zisizo rasmi nchini. Mtafiti kutoka Mbeya, Samuel Kinyondo anabainisha, “Ukosefu wa miundombinu na huduma za msaada ni kikwazo kikubwa katika sekta isiyo rasmi. Bila kushughulikia masuala haya, uwezo wa sekta binafsi hautatumika ipasavyo.”

Changamoto nyingine kubwa ni ukosefu wa ulinzi wa kijamii kwa wafanyakazi wasio rasmi. Tofauti na ilivyo kwa wenzao katika sekta rasmi, wafanyakazi wasio rasmi hawana fursa ya kupata manufaa kama vile bima ya afya, pensheni au likizo ya malipo. Hali hii huwaacha katika mitanziko ya kiuchumi inayopunguza uwezo kuwekeza
katika biashara zao.

Mwonekano sekta isiyo rasmi
Kimsingi, sekta isiyo rasmi itazidi kubakia kuwa sehemu muhimu ya uchumi wa Tanzania kwa siku zijazo. Kwa kutumia sera zenye mwelekeo, miundombinu bora na mifumo imara ya msaada, sekta isiyo rasmi inaweza kuchochea zaidi ukuaji wa uchumi jumuishi hivyo, kuchangia zaidi katika maendeleo ya taifa.

Ili kufikia hatua hii, juhudi za pamoja zinahitajika kutoka serikalini, sekta binafsi na mashirika ya kiraia kushughulikia vikwazo vya kimfumo kama upatikanaji wa fedha, uwepo wa miundombinu duni na vikwazo vya kiudhibiti.

Kwa msingi huo, namna sahihi kushughulikia suala hili ni kufanya uboreshaji wa kodi. Kwa kiasi kikubwa, kwa sasa sekta hiyo inafanya kazi nje ya mfumo wa kodi. Jambo hili linapunguza mapato ya serikali na kuzidi kuiweka
pembezoni sekta hiyo.

Kwa kutunga sera shirikishi za kodi zinazoendelea, serikali itaziwekea biashara zisizo rasmi njia ya kuingia katika
uchumi rasmi bila kuzielemea. Uboreshaji huo ujumuishe taratibu rahisi za kodi, vivutio (motisha) katika kurasimisha na kuhamasisha matumizi ya nyenzo za kidijiti ili kurahisisha ukusanyaji kodi.

Hatua hizi si tu kwamba zitaongeza wigo wa vyanzo vya kodi, bali pia zitatoa fursa kwa wafanyakazi wasio rasmi
kupata ulinzi wa kijamii na huduma za serikali, hivyo kuchochea utulivu na ukuaji wa uchumi.

Victor Tesha anahitimisha akisema, “Sekta isiyo rasmi si tatizo linalohitaji utatuzi, bali ni fursa inayostahili
kuchangamkiwa na kutumiwa ipasavyo. “Kwa kutatua changamoto zilizopo na kutumia nguvu zake, Tanzania inaweza kufungua neema na uwezo kamili wa sekta hii muhimu.”

Kwa msingi huo, mbinu ya kiujumla inayohitajika ni ile inayochanganya uvumbuzi wa kiteknolojia, maendeleo ya miundombinu pamoja na uboreshaji wa sera.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *