SERA ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995 (Toleo la 2023) itaendelea kudumisha kanuni sita za Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995.
Kwa mujibu wa sera hiyo, ardhi ina thamani na itatambuliwa katika miamala ya ardhi. Pia, sera hiyo inatambua kuwa ardhi yote ni ya umma na imekabidhiwa kwa Rais akiwa ni mdhamini kwa niaba ya raia wote.
Kanuni nyingine katika sera hiyo ni kwamba haki ya kumiliki na kutumia ardhi iliyopatikana ama kwa kumilikishwa na serikali au kimila ndiyo mifumo pekee ya kumiliki ardhi itakayotambuliwa.
Pia sera hiyo inaeleza Kamishna wa Ardhi ataendelea kuwa mamlaka pekee ya utawala wa ardhi nchini.
“Kwa madhumuni ya usimamizi, ardhi ya umma itakuwa katika aina tatu ambazo ni Ardhi ya Hifadhi, Ardhi ya Kijiji na Ardhi ya Jumla,” inaeleza sera hiyo.
Inaongeza: “Raia wa Tanzania ndiye atakayekuwa na haki ya kumiliki ardhi nchini na wasio raia watapata ardhi kwa ajili ya uwekezaji pekee”.
Sera inaeleza ardhi ni nguzo kuu ya shughuli za kiuchumi na kijamii na ni rasilimali ya msingi kwa maendeleo ya nchi. Inaeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa inatambua umuhimu wa sekta ya ardhi kuwa ni nguzo muhimu kwa ukuaji wa uchumi, usawa wa kijamii na uendelevu wa mazingira.
Inaeleza kuwa usimamizi na matumizi bora ya rasilimali ardhi yana athari chanya katika sekta mbalimbali zikiwemo sekta za uzalishaji na huduma za jamii.
“Mathalan, takribani asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo hivyo kuifanya ardhi kuwa nyenzo muhimu kwa ukuaji wa uchumi. Kadhalika, sekta ya ardhi ina fursa kubwa ya kuchangia mapato ya serikali na kuwezesha upatikanaji wa ajira,” inaeleza sera hiyo.
Inaongeza: “Vilevile, Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 yanalenga katika kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2030 pamoja na mambo mengine, kunakuwa na miji na maendeleo ya makazi ambayo ni jumuishi, salama, stahimilivu na endelevu”.
Sera inaeleza kuwa mfumo wa umiliki ardhi nchini umeendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kuwezesha ujenzi wa viwanda, makazi, kilimo na ufugaji.
Kwa mujibu wa sera hiyo, mipango ya kitaifa na kimataifa inahimiza kujenga uchumi shindani na wa viwanda kwa maendeleo ya watu na katika sekta ya ardhi inalenga kuendeleza upangaji, upimaji na umilikishaji wa maeneo ya makazi, biashara, uwekezaji na huduma za jamii na hivyo, kuimarisha usalama wa milki na kukuza Pato la Taifa.
“Aidha inalenga kupima ardhi katika maeneo ya mipaka ya nchi na kuzijengea uwezo mamlaka za serikali za mitaa kwa kuzipatia rasilimali fedha, watu na vifaa vya kisasa vya upimaji ardhi na usanifu wa ramani na kuwapatia mafunzo stahiki watalaamu wa ardhi,” inaeleza sera hiyo.