‘Serikali imeanza ujenzi wodi mpya 35 za watoto’

DAR ES SALAAM; NAIBU Waziri wa Afya,Dk Florence Simizi, amesema serikali imeanza hatua ya utekelezaji wa ujenzi wodi mpya 35 za watoto wachanga nchini, ambapo 15 zitakuwa katika hospitali za mikoa na 20 katika hospitali za halmashauri.
Akizungumza wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, ilipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Amana jijini Dar es Salaam, Dk Samizi amesema ujenzi wa wodi hizo utakamilika ndani ya miezi sita.
Aidha amesema Rais Samia Suluhu Hassan amewekeza kwa kiasi kikubwa katika wodi za watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda wao (NICU), ambapo mwaka 2021 walikuwa na wodi 14 tu za NICU nchini, lakini kufuatia maelekezo ya Shirika la afya Duniani (WHO) kwamba kila hospitali iwe na wodi ya watoto wachanga, serikali imefanya uwekezaji mkubwa.
“Leo hii tuna wodi 362 za huduma kwa watoto wachanga nchini, na lengo ni kufikia zaidi ya wodi 500 ili kuhakikisha kila hospitali inayotoa huduma za uzazi inaweza pia kuwahudumia watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao,” amesema Naibu Waziri



