Serikali ya ahidi kuendelea kuwekeza TAZARA

SERIKALI imesema imetenga zaidi ya Sh bilioni 12 katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa utoajki huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo kupitia Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Atupele Mwakibete amesema TAZARA imekuwa ikisafirisha mizigo wa Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hivyo ili kuongeza idadi ya mizigo Serikali imeendelea kutenga fedha kila mwaka ili kuboresha miundombinu hiyo.

“Nchi zinazo tuzunguka zinatumia sana reli hii, na wateja hawa ni muhimu sana kuendelea kuwashawishi kutumia reli hii.

Tusisahau biashara ni ushindani hivyo lazima tuliweke hili la maboresho kama kipaumbele,” amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Mwakibete amesema pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali, ameitaka TAZARA kuhakikisha inafanya ukarabati wa mara kwa mara wa stesheni zao nchini ili kupunguza changamoto zilizopo ikiwemo upungufu wa viti vya kukalia abiria wanaposubiri kuingia kwenye treni.

Aidha, Naibu Waziri Mwakibete amesema ili mgodi wa Kongolo kujiendesha kwa faida ni wakati muafaka kwa TAZARA kuwa na mpango Madhubuti wa biashara ili kutumia vifaa vinavyonunuliwa kwa tija.

Mbunge wa Kyela na Katibu wa Wabunge wa Mkoa wa Mbeya, Ally Jumbe ameipongeza TAZARA kwa kuendeleza juhudi za mara kwa mara za ukarabati kwenye njia na kuhakikisha kuwa treni zinakuwepo na kuondoka kwa wakati.

Meneja wa TAZARA Mkoa wa Tanzania Fuad Abdalla amesema miongoni mwa mikakati ambayo imeendelea kuchukuliwa ili kuongeza ufanisi na kuongeza pato ni pamoja na Mamlaka kuingia makubalino maalum na makampuni binafsi ikiwemo kampuni ya Calabash ili kuhakikisha kuwa reli hiyo inatumika wakati wote.

Fuad ameongeza kuwa TAZARA pamoja na changamoto za uchache wa vichwa vya treni na behewa Mamlaka imeendelea kuhakikisha inatumia vizuri miundombinu iliyopo kwa kutoa huduma za viwango kwa kusafirisha abiria na mizigo kwa wakati.

Naibu Waziri Wa Uchukuzi Atupele Mwakibete yuko Mkoani Mbeya kwa ziara ya siku tatu kukagua miradi na miudnombinu inayotekelezwa na kusimamiwa na Sekta hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button