Serikali kufungua Kanisa la Ufufuo na Uzima

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, ameagiza kufunguliwa kwa Kanisa la Ufufuo na Uzima pamoja na kukiweka chini ya uangalizi wa miezi sita ili kuhakikisha linafuata miiko, masharti na sheria za uendeshaji wa taasisi za kidini.
Amesema adhabu kwa makosa ya viongozi wa taasisi za dini haipaswi kuathiri waumini na haki yao ya kuabudu, hivyo sharti lililokuwa likitaka kufungwa kwa nyumba ya ibada iwapo kiongozi atakosea lirudishwe upya ili adhabu itolewe kwa mhusika mwenye makosa.
“Natambua ilikuwepo hii moja ya Ufufuo na Uzima, kaifungulie. Wape masharti ya uangalizi ndani ya miezi sita. Ziandikie taasisi zote za kidini kuzikumbusha miiko na mipaka ya ufanyaji kazi sawa na sheria na Katiba ya nchi yetu,” amesema.
Kanisa hilo lilifutiwa usajili Juni 2 mwaka huu kutokana na madai ya kukiuka masharti ya uendeshaji wake kwa kuingiza masuala ya kisiasa katika utumishi wake. Serikali imesisitiza kuwa hatua hiyo ina lengo la kulinda nidhamu, ustawi na uwajibikaji katika usimamizi wa taasisi za kiroho.
Kauli ya Waziri Mkuu imetolewa Jumatatu, Novemba 24, 2025, wakati akihutubia mkutano wa hadhara baada ya ziara ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025. SOMA: Dk. Mwigulu akagua uharibifu wa vurugu



