Serikali yahimiza ushirikiano sera za uchumi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba

SERIKALI imehimiza washirika wa maendeleo waendelee kuunga mkono juhudi za serikali kutekeleza sera za kiuchumi kwa maendeleo endelevu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alisema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa majadiliano ya kimkakati kati ya serikali na washirika wa maendeleo.

Tutuba alisema serikali inatambua na kuthamini michango yao kwa kuwa inaamini mafanikio na maendeleo ya uchumi yanategemea michango na matokeo ya majadiliano hayo yataiwezesha nchi kufikia malengo yake ya ukuaji uchumi.

Advertisement

Mkutano huo ulijadili mada kadhaa ikiwamo ya uchumi wa taifa kwa ujumla na masuala ya mazingira kwa kuangalia changamoto ya kimazingira na tabianchi.

Wakati akifungua mkutano huo, Makamu wa Kwanza wa Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman alihimiza washirika wa maendeleo kushiriki kuwezesha nchi kufufua fursa za kiuchumi zilizozuiwa na kuharibiwa na athari za Covid-19 na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine.

Othman alisema serikali inatambua michango iliyotolewa na washirika hao, lakini bado inahitaji ushirikiano katika kuiwezesha nchi kufikia malengo yake.

“Wote tunajua uchumi wa dunia kwa mwaka 2022, umetikiswa na vita baina ya Urusi na Ukraine, hii imetokea katika kipindi ambacho nchi nyingi duniani zilikua zimeanza kuimarika kutoka katika janga la corona, Tanzania Bara na Zanzibar pia ni miongoni mwa nchi zilizoathirika kwa kuwa inategemea wawekezaji na ushirikiano wa wadau wa maendeleo,” alisema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Saada Salim Mkuya alisema mkutano huo ungejadili namna ya kuiwezesha nchi kutumia rasilimali zilizopo kwa ajili ya kukuza uchumi.

Mwenyekiti Mwenza wa washirika wa maendeleo nchini, Zlatan Milisic alisema wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika majadiliano yanayohamasisha uwazi na uwajibikaji kwa maendeleo ya Watanzania.

Milisic aliipongeza serikali kwa kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi ambayo matokeo yake yatatumika kwa maendeleo ya kiuchumi.

Aidha, aliipongeza serikali kwa kuwa na uongozi unaozingatia haki za binadamu na jitihada inazozichukua kuboresha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.