Serikali yatoa trilioni 3.5/-kuwezesha vijana kiuchumi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali imefanikiwa kutoa Sh trilioni 3.5 kufi kia mwaka 2024 kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana kiuchumi kutoka Sh bilioni 904 mwaka 2021.
Amesema fedha hizo zimewasaidia vijana kupata mitaji ambayo imewawezesha kushiriki shughuli za uzalishaji mali na kuinua vipato vyao pamoja na uchumi wa taifa.
Amesema hayo wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa iliyofanyika mkoani Mbeya.
SOMA: Kongani kukuza ujuzi kwa vijana
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni ‘Nguvu Kazi ya Vijana kwa Maendeleo Endelevu.’
Majaliwa amesema serikali imefanya hivyo kwa kutambua kuwa vijana ni nguvu kazi na ndiyo msingi wa safari ya maendeleo ya taifa.
“Vijana wakipewa nafasi na kuandaliwa ipasavyo, wanaweza kuwa nguzo kuu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs),” amesema.
Majaliwa ameongeza kuwa vijana wamekuwa nguzo muhimu ya maendeleo katika sekta mbalimbali nchini na wamechangia kwa kiwango kikubwa katika kilimo, biashara, teknolojia, michezo na sanaa.
“Katika nyanja za ubunifu na teknolojia, vijana ndiyo vinara wa matumizi ya teknolojia mpya na majukwaa ya kidijiti, ikiwemo akili mnemba na mifumo ya mawasiliano ya kisasa, michango yao imekuwa kichocheo cha mabadiliko chanya katika jamii na uchumi wa taifa,” amesema.
Ametoa mwito kwa wadau wote kuhakikisha vijana wanashirikishwa kikamilifu katika ngazi zote za maamuzi na si tu kama wanufaika wa sera, bali pia kama wabunifu na viongozi wa mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza alipotembelea banda la VETA, Majaliwa ametoa mwito kwa taasisi hiyo pamoja wadau wengine wa elimu kuwapa kipaumbele cha mafunzo watu wenye ulemavu pamoja na kuwaandalia nyenzo muhimu za kujifunzia ili waweze kutumia ujuzi watakaoupata kuongezea kipato.
“Baada ya kutembelea banda hili nimejifunza wapo vijana wenye ulemavu wana ujuzi na vipaji, wazazi tuwe tayari kuwatoa watoto wetu wenye ulemavu na taasisi za elimu ziwapokee na kuwapa ujuzi,” amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa kundi la vijana na ndiyo maana inawekeza na kuthamini mchango na nguvu zao katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
“Hii ni rasilimali kubwa ambayo ikielekezwa na ikijengewa uwezo ipasavyo kupitia vipaji walivyonavyo italeta maendeleo endelevu, kujenga taifa shindani na lenye ustawi,” amesema.