Takukuru ‘ikaze buti’ taifa lipate viongozi bora

TANZANIA inaelekea kufanya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Huo ni uchaguzi muhimu kwa Watanzania kwa kuwa viongozi watakaochaguliwa ndio watakaoamua mustakabali wa Tanzania ijayo. Kwa msingi huo, wananchi wanapaswa kuwa makini na kuchagua viongozi waadilifu wasiokubali kutoa wala kupokea rushwa nyakati zote, zikiwamo za uchaguzi.

Ndiyo maana hata juzi wakati akitoa salamu za pole kwa familia ya aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Cleopa Msuya na wananchi wa Mwanga mkoani Kilimanjaro, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda anatoa mwito kwa wananchi kutokubali kuhadaiwa na watu wanaotafuta madaraka kwa kutoa rushwa.

Katika tukio hilo kutokana na kifo cha Msuya aliyezikwa jana, Pinda anasema: “Viongozi wetu wametuasa, tuwakatae wanaogawa vihela huku na huko ili waje watuhudumie. Sasa kama nia yako ni kutoa huduma una haja gani ya kutoa rushwa? Sisi tutakupima kwa kazi utakayoifanya…”

Akizungumza katika ufunguzi wa warsha ya wadau wa habari hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispin Chalamila anahimiza wananchi kutochagua viongozi ‘wanaoabudu’ kutoa na kupokea rushwa.

Anasema kufanya kosa hilo kutawagharimu kwa kupata viongozi wasio waadilifu. “Waandishi wa habari fanyeni habari za uchunguzi na kufichua vitendo vya rushwa kusaidia mapambano haya ili wanajamii wasipitishe  viongozi wanaotokana na rushwa,” anasema Chalamila.

Kwa mujibu wa Chalamila, Takukuru ni mamlaka huru inayofuata misingi ya sheria na uadilifu na kamwe, haiwezi kubagua wala kupendelea wanaojihusisha na vitendo vya rushwa ama iwe kabla, wakati au baada ya uchaguzi.

Kinachopendeza ni kwamba, hadi sasa Takukuru inaendelea kujipanga na kuingia katika ‘machimbo ya wanaoabudu’ rushwa kwa kuendelea kuchunguza taarifa kuhusu rushwa katika mchakato na matukio mbalimbali yanayohusu uchaguzi mkuu ujao.

Kwamba, Takukuru waendelee kuwa imara wakijua kuwa kadiri muda unavyokaribia mchakato na hata
wakati na baada ya uchaguzi, wapo wenye nia mbaya ambao watatumia kila njia wawezayo kuinyong’onyesha
taasisi hii na kuikatisha tamaa ili isifanye kazi zake vizuri na wao waendelee kupenya na kujificha katika uovu huo
unaopora haki za watu.

Kwa msingi huo, Tanzania inapoelekea uchaguzi huo, kila Mtanzania aoneshe uzalendo wake kuliko kipindi chochote kilichopita. Kila mmoja auone wajibu mbele yake kufichua kila aina ya uovu au uhalifu wa kisiasa, ukiwamo wa matumizi ya rushwa kupata uongozi ama iwe rushwa ndogo, au kubwa.

Akizungumza na HabariLEO Mkuu wa Takukuru katika Mkoa wa Temeke, Joseph Makungu anasema zipo taarifa kadhaa kuwa, wapo baadhi ya watia nia wanaojaribu kujihusisha na vitendo vya rushwa ili wapitishwe na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao.

Anasema wanaendelea kuchakata taarifa hizo na kuzifanyia uchunguzi kubaini ukweli na kuchukua hatua stahiki za kisheria. Kimsingi katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 wadau wanataka Takukuru itumie nguvu kubwa bila kuchoka, kufikia zaidi jamii na kuipa elimu endelevu juu ya madhara ya rushwa katika uchaguzi kiuchumi na hata kijamii.

Hili linatiwa nguvu na kauli ya Makungu anayesema: “…Tunazo idara za intelijensia ambazo zipo huko ndani lakini pia wananchi tumekuwa tukiwaelimisha kwamba anayekumbana na changamoto za namna hiyo (kudaiwa rushwa au kushawishiwa kupokea rushwa) atupe taarifa.”

Anaongeza: “Wakati mwingine waandishi wa habari tunawaona kama mhimili wa nne, taarifa zenu kupitia magazeti, redio na kadhalika zikizungumzwa mahali fulani tunaenda kuchukua hatua, lakini uelimishaji umma pia tumeuwekea kipaumbele.

“Kanuni ya 25 (6) inaeleza nani wanaweza wakatekeleza majukumu yao; inawazungumzia waliopo madarakani
kama wabunge waliopo sasa, madiwani, wawakilishi wa Zanzibar na inamzungumzia pia Rais”.

Anaongeza: “Hizi ni zile kanuni za chama tawala, kama kuna mtu amekiuka wakati mwingine tunampeleka  kwenye chama hicho hicho ambacho kanuni zake zimekiukwa ili hatua zichukuliwe dhidi ya huyo mkiuka sheria au kanuni.”

Ndiyo maana katika kuelekea uchaguzi, asiwepo Mtanzania yeyote atakayedanganywa ama kwa kuombwa au kupewa na yeyote kupokea rushwa maana rushwa ni adui wa haki na pia, asiwepo atakayekubali kuuza, kununua, kuazima au kuazimisha kadi yake maana yote hayo sambamba na rushwa, ni makosa katika uchaguzi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button