TAKUKURU Tanga yaokoa Mil 76/-makusanyo ya mapato

Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Tanga, Ramadhani Ndwatah.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mkoani Tanga imeokoa sh Milioni 76.04 kutokana na ubadhirifu wa fedha za mapato ya serikali kwa mfumo wa POS uliofanywa na watumishi wa umma katika wilaya za Kilindi, Korogwe na Tanga Jiji.

Mkuu wa TAKUKURU Tanga, Ramadhani Ndwatah amesema hayo wakati akitoa taarifa za utendajikazi wa taasisi hiyo katika kipindi cha Octoba hadi Disemba 2024.

Amesema TAKUKURU imewafikisha mahakamani watumishi hao na waliamuriwa na Mahakama kurejesha fedha hizo ambazo ni mali ya umma.

Advertisement

Akitoa mchanganuo wa fedha hizo amesema katika wilaya ya Kilindi sh milioni 58.6 zimerejeshwa baada ya kushinda kesi ya uhujumu uchumi dhidi ya watumishi ambao walishtakiwa kutowasilisha fedha za mapato ya serikali ambazo zilikusanywa kwenye mfumo wa POS.

Kwa upande wa wilaya ya Korogwe sh milioni 9.1 ambazo ni mapato ya serikali yaliyokusanywa kwenye mfumo huo zimerejeshwa.

“Kwa Tanga Jiji kiasi cha sh Mil 3.1 ziliweza kurejeshwa baada ya kufanyika ubadhirifu kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu na mikopo ya asilimia 10,”amesema Ndwatah.

Aidha Mkuu huyo wa TAKUKURU amesema kuwa katika kipindi hicho taasisi hiyo ilifanya ufuatiliaji na ukaguzi kwenye miradi 42 ya maendeleo yenye thamani ya sh bilioni 15.4.

Amesema kuwa walibaini mapungufu kwenye miradi 24 yenye thamani ya sh bilioni 13.9 na kuwajulisha wahusika na kuwashauri kuyafanyia kazi mapungufu hayo ili kuondoka dosari zilizokuwepo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *