Tamisemi yataka shule zaidi tahasusi za sayansi

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa ameitaka mikoa na wadau wa elimu kuendelea kuongeza tahasusi katika shule za kidato cha tano hususani za masomo ya sayansi.

Akizungumza wakati wa kutoa taarifa kwa umma kuhusu uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga kidato cha tano, vyuo vya elimu ya ufundi kwa mwaka 2025 jijini Dodoma, Mchengerwa amesema mikoa na wadau wa elimu wanapaswa kuongeza tahasusi za masomo ya sayansi ili kutoa fursa ya wanafunzi wengi kujiunga na masomo ya sayansi.

“Mikoa na wadau wa elimu hakikisheni mnakuwa na tahasusi zote za msingi katika shule zake ili kuwapunguzia wazazi na walezi na wanafunzi gharama za usafiri kwenda shule za mbali,” alieleza Mchengerwa.

Mchengerwa pia amewataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wadau wa elimu kuhakikisha wanatekeleza azma ya serikali ya kuwa na shule ya sekondari ya kidato cha tano katika kila tarafa.

“Nitumie fursa hii kutoa wito kwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa azma ya serikali ya kuwa na shule za sekondari za kidato cha tano katika kila tarafa inatekelezwa, ili kuwezesha wanafunzi wote wanaofaulu mtihani wa kidato cha nne kupata nafasi ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita,” alisema Mchengerwa.

Aidha, alihimiza viongozi hao kuendelea na upanuzi na ujenzi wa shule mpya za kidato cha tano na sita katika maeneo yao na kuongeza tahasusi za masomo ya sayansi.

Aliwashukuru viongozi na watendaji wa mikoa na mamlaka za serikali za mitaa na wadau wa elimu na wananchi kwa kushiriki kikamilifu kuimarisha miundombinu ya shule ikiwamo ujenzi wa madarasa, mabweni na majengo mengine yaliyowezesha shule kupokea wanafunzi wote waliopangwa kujiunga na kidato cha tano.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button