Tanesco yaruhusu ubia uzalishaji umeme

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limezindua Mfumo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Tanesco (TIMS), unaowawezesha wawekezaji na taasisi binafsi kuingia ubia na shirika hilo katika kutekeleza miradi mikubwa ya uzalishaji umeme nchini.
Uzinduzi huo umefanywa Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga na kusema mfumo huo unaruhusu wawekezaji kujisajili na kuwasiliana na shirika katika kuingia ubia wa kutekeleza miradi ya uzalishaji umeme.
Alisema hatua hiyo ni kubwa na kuipongeza Tanesco kwa hatua hiyo ya kutumia wataalamu wake wa ndani kubuni mfumo huo wa Tehama ambao utaongeza ufanisi wa shirika na kupunguza urasimu.
“Uzinduzi huu ni utayari wa Tanesco kushirikiana na sekta binafsi kutekeleza miradi mikubwa ya uzalishaji umeme na tayari miradi minne imeshaingia kwenye mfumo huu,” alisema Kapinga.
Kapinga alisema mfumo huo ni mwendelezo wa safari ya kidijiti ndani ya shirika hilo, lakini pia ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali ya kutaka matumizi ya mifumo inayosomana kama njia ya kurahisisha utoaji huduma na kuongeza ufanisi wa kazi.
“Niwapongeze kwa hatua hii kubwa ya kuja na mfumo huu ambao wawekezaji wanaingia kuangalia fursa za uwekezaji kwenye nishati na kuzichangamkia kwa kuona maeneo ya kuwekeza kuzalisha umeme,” alisema.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange akizungumzia mfumo huo alisema una faida nyingi na baadhi yake ni kuongeza uwazi, kupuguza urasimu kwa wawekezaji, urahisi wa kupata taarifa na fursa za uwekezaji na kuongeza tija kwenye ya utoaji huduma.
“Mfumo huu mpya utatusaidia kupima jinsi tunavyotoa huduma zetu na hii itaongeza tija na kuleta ufanisi
wa matumizi ya Tehama,” alisema.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mipango, Utafiti na Uwekezaji wa Tanesco, Renata Ndege alisema TIMS ni kichocheo cha ufanisi ndani ya shirika hilo lakini ni mfumo salama na rahisi kuutumia.
Alisema uzinduzi wake ni sehemu ya mkakati wao wa muda mrefu ndani ya shirika katika kuboresha matumizi
ya teknolojia ya habari na mawasiliano.