Tanga sensa ni shwari

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Omar Mgumba amesema hadi sasa sensa ya watu na makazi inaendelea vizuri mkoani kwake na ameomba wananchi ambao hawajafi kiwa wawe wavumilivu.
Mgumba alisema jumatano kuwa hajapokea changamoto yoyote zaidi ya kuwa bado kuna wananchi ambao hawajafikiwa na makarani kwenye maeneo mengi mkoani hapa.
Alisema sababu za kutofikiwa ni pamoja na ugeni wa teknolojia inayowafanya wakati mwingine makarani kufanya kazi hiyo kwa kasi ndogo.
“Tunaomba ambao hawajafikiwa waendelee kuvumilia kwa kuwa bado tuna siku sita (tano) za kufanya kazi hii na watakapofikiwa na makarani, wawape ushirikiano ili tumalize vizuri,” alisema Mgumba.
Aliwaasa wamiliki wa shule za binafsi wazingatie utaratibu uliowekwa wa kuzifunga shule ili kupisha sensa iendelee kufanyika kama ilivyopangwa.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashim Mgandilwa alisema shughuli hiyo imeendelea kutekelezwa kwa ufanisi, tangu wakati wa mafunzo kwa makarani mpaka sasa hakujatokea kikwazo kutoka kwa wananchi wala makarani.
“Wananchi wamekuwa na mwitiko mzuri na makarani wanazingatia utaratibu kutimiza majukumu yao vizuri… Bado hatujapokea dosari ya aina yoyote zaidi ya malalamiko ya makarani kutofika katika baadhi ya maeneo, hatua ambayo nina imani wataweza kufikiwa kwani siku bado zipo,” alisema Mgandilwa



