Tano zafuzu robo fainali kikapu Dar

TIMU tano za mpira wa kikapu zimefuzu hatua ya robo fainali Ligi ya mkoa wa Dar es Salaam baada ya kumaliza mzunguko wa mechi 30 zikiwa zinazoongoza kwa kufanya vizuri.

Zilizofuzu ni Dar City iliyomaliza kinara kwa pointi 57, UDSM Outsiders pointi 55, JKT pointi 53 sawa na Savio katika nafasi ya nne na Srelio iliyoko nafasi ya nane kwa pointi 45.

Advertisement

Timu tatu ambazp ziko kwenye nane bora zinazosubiri kumaliza mzunguko wa mwisho ili kujiunga na wenzao ni Mchenga pointi 50, ABC pointi 46 na Vijana pointi 45.

SOMA: DC Ilala apongeza ujenzi Uwanja wa Kikapu

Timu nane za juu ndizo zitakazoingia hatua hiyo ya mtoano ambapo kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Ufundi na Mashindano wa Chama Cha Mpira wa Kikapu Dar es Salaam Haleluya Kavalambi, michezo ya kufunga mzunguko itamalizika mwishoni mwa wiki hii.

Michezo ya hatua ya mtoano kwa timu nane itaanza Oktoba 8 hadi Oktoba 31 ambapo atapatikana bingwa wa jumla ya Ligi hiyo.

Timu ambazo ziko hatarini kushuka daraja ni Kampala International University(KIUT), Jogoo na Crows.

Wachezaji wanaoongoza katika ufungaji bora ni wengi ila watatu wenye pointi nyingi ni Stanley Mtunguja wa Ukonga Kings mwenye pointi 539 akiongoza pia kwa kuchangia pasi za mabao kwa pointi 158 akifuatiwa na Amina Juma wa Mchenga Queens pointi 524 na pasi pointi 136 na nafasi ya tatu ni Jonas Mushi wa JKT pointi 512.