Tanzania, Msumbiji wageukia uchumi

RAIS Samia Suluhu Hassan amemuaga mgeni wake Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo aliyewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Hafla ya kumuaga ilifanyika Ikulu Dar es Salaam kwa gwaride maalumu lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo wakuu wa majeshi ya ulinzi na usalama.
Msafara wa Rais wa Msumbiji ulipowasili katika viwanja vya ikulu, ulipokewa na mwenyeji Rais Samia na moja kwa moja walielekea kwenye eneo maalumulililoandaliwa kwa ajili ya kuagwa.
Katika hafla hiyo, wimbo wa Taifa la Tanzania uliimbwa pamoja na wa Msumbiji.
Akiwa Zanzibar, Rais Chapo amesema nchi yake ina dhamira ya dhati kushirikiana na Tanzania kutokana na kuwepo kwa undugu wa asili wa muda mrefu, ambapo sasa unatakiwa kujikita zaidi katika mageuzi makubwa ya kiuchumi.
Akiwa Ikulu ya Zanzibar alifanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi katika ziara ya siku moja Zanzibar iliyomuwezesha kutembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo maeneo huru ya kiuchumi na uwekezaji Fumba.
Alisema amefurahishwa na ziara ya kutembelea Zanzibar ambapo Msumbiji inaweza kujifunza mambo mengi, ikiwemo umuhimu wa kutenga maeneo huru ya kiuchumi kwa ajili ya uwekezaji.
Alisema ushirikiano huo unahitajika ambapo baada ya harakati za muda mrefu za ukombozi wa wapigania uhuru huu ni wakati wa kujikita katika uwekezaji na uchumi.
Alisema huu ni wakati wa kuingia katika mageuzi makubwa ya sera za mambo ya nchi za nje ya mataifa hayo kutoka kupigania uhuru hadi mageuzi ya kiuchumi kwa masilahi ya wananchi wake.
“Nimefurahishwa na ziara ya kutembelea Zanzibar ambapo nimejifunza mambo mengi, ikiwemo maeneo huru ya kiuchumi yaliyopo Fumba pamoja na bandari ambapo ni fursa muhimu za uwekezaji na kuingiza mapato,” alisema.
Akizungumza Rais wa Zanzibar, Dk Mwinyi alisema Zanzibar ina fursa ya kujifunza mambo mbalimbali yaliyopo Msumbiji, ikiwemo maendeleo ya mafuta na gesi.
Alisema nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika uwekezaji wa nishati hiyo kwa muda mrefu huku Zanzibar ikiwa ipo katika mageuzi ya utafutaji na uwekezaji wa mafuta na gesi.
Aliyataja maeneo mengine waliyozungumza ni mikakati ya kuimarisha sekta ya utalii, ikiwemo kubadilishana uzoefu na wataalamu katika pande mbili hizo.
“Tumezungumza na wenzetu wa Msumbiji katika biashara na uwekezaji wa nishati ya mafuta na gesi ambao kwa bahati nzuri wenzetu wamepiga hatua kubwa kwa zaidi ya miaka 20, pia tumekubaliana katika mikakati ya kuimarisha sekta ya utalii,” alisema.
Katika ziara hiyo, Tanzania na Msumbiji zilisaini mikataba miwili na hati nne za makubaliano ili kuboresha uhusiano kati ya mataifa hayo na miongoni mwa mikataba hiyo ni Mkataba wa makubaliano ya uanzishwaji wa kituo cha pamoja cha mpakani kati ya Tanzania na Msumbiji cha Mtambaswala.
Pia, walisaini mkataba wa kubadilishana wafungwa na hati nne za makubaliano ya ushirikiano, ikiwemo ya makubaliano ya kubadilishana wanafunzi kati ya Tanzania na Msumbiji.
Aidha, nchi hizo zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika biashara na uwekezaji, kuwawezesha wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati ili wafanye biashara kwa urahisi.
Rais Samia alisema wamekubaliana kuharakisha uanzishwaji wa vituo vya pamoja vya mpakani ili kuondoa shida wanazopata wananchi wa pande zote.