TSN kuongeza uelewa wa Umma AFCON 2027

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali (TSN) imepanga kuandaa na kuchapisha makala maalumu zitakazolenga kuhabarisha umma kuhusu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, hatua inayolenga kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika tukio hilo kubwa la kimataifa.

Sambamba na hilo, shirika hilo litaendelea kuelimisha umma juu ya mipango, miongozo, mikakati, sera pamoja na miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali, kwa lengo la kuongeza uwazi na uelewa wa shughuli za maendeleo.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda ametoa taarifa hiyo leo Mei 4, 2026 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27 bungeni jijini Dodoma.

Katika kuimarisha usambazaji wa habari, TSN imepanga kuchapa na kusambaza jumla ya nakala 1,909,752 za magazeti yake ya Daily News na HabariLEO ndani na nje ya nchi. Pia kukamilisha mradi wa ukarabati wa studio ya kisasa ya kidigitali, itakayosaidia kuongeza ubora wa uzalishaji wa maudhui na kuendana na mabadiliko ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

Kwa upande wa kidigitali, TSN imepanga kuandaa maudhui mbalimbali na kuyasambaza kupitia chaneli ya Daily News Digital pamoja na mitandao ya kijamii, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwafikia wasomaji wengi zaidi kwa njia za kisasa.

Kwa upande wa rasilimali watu, TSN imepanga kuwezesha mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi 130 na mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi 18, ili kuongeza ujuzi na tija katika utoaji wa huduma.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button