Tume ya TEHAMA yabainisha fursa kupitia NaPA

DODOMA: TUME ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) imewataka wabunifu nchini kutumia fursa za mfumo wa anuani za makazi na kubuni huduma mbalimbali za kidigitali kwani zitawafikia Watanzania wote popote walipo.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Tehama, Dk Nkundwe Mwasaga, wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya Mfumo wa Anuani za Makazi, Alhamis (Februari 6, 2025) jijini Dodoma.

Dk Mwasaga amesema mfumo wa NaPA umefungua milango ya fursa kwa wabunifu wa bidhaa za Tehama kuanzisha suluhisho za kisasa, ambazo zitabadilisha njia za utoaji huduma katika jamii.

Advertisement

Alisema kuwa mfumo wa Anwani za Makazi ni nyenzo ya utambuzi ambayo inarahisisha utoaji na upokeaji wa huduma mbalimbali ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, mapinduzi ya 4,5 na 6 ya viwanda yanategemea matumizi ya TEHAMA hivyo ushiriki wa Tume hiyo katika kutoa elimu kwa Watanzania ni moja ya jukumu lake kwa lengo la kuhakikisha kuwa uwepo wa mifumo hiyo inaleta manufaa kwa Watanzania wote.

“Katika maonesho haya, ni muhimu sana kwetu sisi kama Tume, lakini kwa taifa kwa ujumla kuweza kuendelea kuwafikia Watanzania wa mijini na vijijini waweze kufahamu umuhimu wa anuani za makazi kidigitali ili kila mmoja ashiriki katika kuujenga uchumi wa kidigitali,” alisisitiza.

SOMA: Serikali yathibitisha misaada ya Marekani kusitishwa

Alibainisha kuwa uchumi wa kidigitali “ni uchumi wa watu” hivyo ili watu waweze kutumia mifumo kufanya shughuli zao kidigitali, wanahitaji kupata uhakika wa kufikishiwa huduma katika maeneo mbalimbali ikiwemo ofisini, biashara na makazi.

Maadhimisho hayo yaliyozinduliwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa yanaongozwa na kaulimbiu: “Tambua na Tumia Anwani ya Makazi Kurahisisha Utoaji na Upokeaji wa Huduma.

Wizara nyingine zinazoshiriki maadhimisho hayo ni pamoja na Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Katika maadhimisho hayo, taasisi za uma na binafsi zikiwemo Posta, NIDA, UCSAF, TTCL, TCRA, TCRA CCC, NEMC, Tume ya Taarifa Binafsi, “YAS”, NMB na TANAPA zinatoa huduma ya kuelimisha umma juu ya huduma mbalimbali zinazotolewa kupitia anuani za makazi.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *