Tume yakutana viongozi wastaafu

TUME ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imeendelea na vikao vyake leo Februari 6, 2026 kwa kukutana na Mawaziri Wakuu Wastaafu, Kassim Majaliwa na Mizengo Pinda, kwa nyakati tofauti.
Mikutano hiyo imefanyika katika ukumbi uliopo katika Jengo la Takwimu mkoani Dodoma, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Tume kukusanya taarifa, maoni na ushauri kutoka kwa viongozi wakuu wa zamani kuhusu matukio hayo.
Katika mkutano na Waziri Mkuu Mstaafu Kassim Majaliwa, Tume ilijadili kwa kina namna matukio ya uvunjifu wa amani yalivyoanza, athari zake kwa wananchi, mali zao na miundombinu, pamoja na mapendekezo ya namna ya kudhibiti na kuzuia matukio kama hayo yasijirudie siku zijazo.
Vilevile, katika mkutano mwingine uliofanyika leo, Tume ilikutana na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda ambapo hoja zilizojadiliwa zilihusu maeneo hayo hayo, ikiwemo tathmini ya athari za matukio hayo na ushauri wa hatua za kijamii na kisheria zinazoweza kuchukuliwa ili kuimarisha amani na mshikamano wa kitaifa.

Tume inaendelea kukutana na makundi mbalimbali ikiwemo waathirika wa matukio ya uvunjifu wa amani katika mikoa tofauti nchini, kwa lengo la kukusanya ushahidi na taarifa zitakazoiwezesha kuandaa ripoti ya kina. SOMA: Tume yakutana na Makamu wa Rais Mstaafu
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume, shughuli za ukusanyaji wa taarifa zinaendelea mkoani Dodoma katika Ukumbi wa Takwimu, mkoani Iringa katika Ukumbi wa Siasa ni Kilimo, huku mkoani Shinyanga Tume ikiendelea na kazi zake katika Ukumbi wa Manispaa ya Kahama.
Taarifa zote zitakazokusanywa zitawasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki za kisheria na kiutawala ili kudhibiti na kuzuia vitendo vya uvunjifu wa amani visije kujirudia.



