“Tupo tayari kulipa kodi”

WAFANYABIASHARA ndogondogo maarufu Wamachinga mkoani Dar es Salaam wamesema wako tayari kulipa kodi kwa kadiri ya kipato chao ili kuchangia maendeleo ya nchi.

Hatua hiyo imekuja baada ya viongozi wa wamachinga kukutana na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mkuu wa Wilaya ya Ilala kujadiliana masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kuwapanga wamachinga hao katika Soko la Kariakoo ili liendelee kuwa la Kimataifa.

Akizungumza baada ya majadiliano hayo leo, Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema kuwa kisheria wafanyabiashara wenye mauzo kuanzia Sh milioni nne hadi saba kwa mwaka wanapaswa kuchangia kuanzia Sh 100,000 sawa na Sh 8,300 kwa mwezi.

SOMA: Mbunge alia na mabilioni ya wamachinga

“Kwa wamachinga waliopo Kariakoo wengi wao mauzo yao ni zaidi ya haya hivyo, tutaanza na kiwango cha Shilingi laki moja kwa mwaka na wenye mauzo kuanzia milioni saba anachangia 250,000 sawa na Shilingi 20,800 kwa mwezi,” amesema Mwenda.

Ameeleza kuwa baada ya kuwapanga wamachinga hao wateja wataamua kwenda kununua bidhaa kwa wamachinga au Kariakoo.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Wamachinga Tanzania na Mwenyekiti Soko la Kariakoo, Stephen Lusinde baada ya kufanya mazungu amesema kuwa wamachinga wote wako tayari kulipa kodi ambayo itaendana na uwezo wao.

Amesema kulipa kodi ni uzalendo kwani maendeleo yanayofanywa nchini yanatokana na kodi za Watanzania hivyo, hawako tayari kuona maendeleo bila mchango wa wamachinga.

Lusinde ameeleza kuwa wataanza kutoa elimu ya pamoja kuhusu ulipaji wa kodi na kwamba itawafanya wawe sekta rasmi kwa kuwa wanalipa kodi ya serikali na kuchangia kwenye ujenzi wa taifa.

SOMA: Mpogolo: ‘Machinga’ zingatieni maelekezo

Pia amesema hawako tayari kuwalinda walipa kodi ili kusiwepo na visingizio kwamba wafanyabiashara wakubwa hawalipi kodi kwa sababu yao.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema kuwa mkakati wao ni kuhakikisha Soko la Kariakoo linabaki kuwa la kimataifa kwa kuhakikisha hakuna wamachinga watakaokaa kwenye njia za kuingilia sokoni hapo.

Amesema masoko katika maeneo mbalimbali yanajengwa ili wamachinga waweze kufanya biashara hivyo, wataongeza idadi ya walipa kodi.

“Tunawatengenezea mazingira wamachinga kwani pia wana mchango mkubwa kwenye maendeleo ya nchi, pia lazima tuwaheshimu wafanyabiashara wakubwa,” amesema Mpogolo.

Habari Zifananazo

Back to top button