TZ, Japan kuimarisha biashara ya kaboni

DAR ES SALAAM: Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingara, Mhandisi Cyprian Luhemeja, leo amezindua Kamati ya Pamoja kati ya Tanzania na Japani kuhusu biashara kaboni.
Akizungumza leo Septemba 16, 2025, Mhandisi Luhemeja amesema kamati hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili katika kushughulikia mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuendeleza miradi ya mbali mbali yenye tija kwa taifa.
Aidha, Luhemeja amesema kamati hiyo itarahisisha uratibu na ushauri wa kitaalamu, sambamba na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje katika sekta za nishati safi, kilimo endelevu na uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Japan nchini Tanzania, Ueda Shoichi, amesema kuwa ushirikiano huo unaonyesha dhamira ya taifa hilo kushirikiana na Tanzania katika biashara ya kaboni, teknolojia, uwekezaji na maendeleo endelevu.