KATIKA gazeti la HabariLEO, ipo habari kuhusu majaribio ya kifaa cha usambazaji wa taarifa za hali ya hewa katika Kisiwa cha Goziba, Ziwa Victoria mkoani Kagera yanayofanywa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Taarifa imesema kifaa hicho kinatarajiwa kuwezesha wavuvi na watumiaji kupata utabiri wa hali ya hewa ili kuwaokoa na athari za hali mbaya ya hewa zinazoweza kutokea.
Kwa mujibu wa TMA, kifaa hicho kitawezesha watumiaji wa Ziwa Victoria kwenye kisiwa cha Goziba kuona utabiri wa hali ya hewa mapema na kufanya uamuzi sahihi ili kuokoa maisha na mali zao.
Tunapongeza ubunifu huu wenye manufaa makubwa si tu kwa wavuvi bali na jamii kwa ujumla katika kisiwa hicho na maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria.
Utabiri sahihi wa hali ya hewa una manufaa mengi kwa wananchi hasa katika kipindi hiki ambacho dunia, Tanzania ikiwamo, inakabiliwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Majaribio haya ni muhimu kwa kundi la wavuvi ambao mara nyingi hujikuta wakienda majini (ziwani au baharini)
bila kufahamu kama hali ya hewa ni nzuri au mbaya.
Matukio ya wavuvi kukumbwa na upepo mkali wawapo ziwani au baharini yamekuwapo nchini, tunaamini baadhi
yake hutokana na wavuvi kutokuwa na taarifa ya hali halisi ya hewa.
Mathalani, hivi karibuni wavuvi wapatao 500 kutoka Kata ya Nanganga na Mtowisa waliokuwa wanaendelea na shughuli za uvuvi katika Ziwa Rukwa, walipatwa na dhoruba ya upepo mkali katika Ziwa Rukwa na kusababisha vifo vipatavyo 10.
Kwa hiyo, kama upo uwezekano wa kuwa na kifaa cha namna hiyo (hasa baada ya majaribio), chenye uwezo wa
kusambaza taarifa za hali ya hewa, tunatamani kusikia TMA na wadau hao wakiendelea kuelekeza huduma hiyo katika maeneo mengine nchini.
Itakuwa ni njia nzuri ya wavuvi na jamii kwenye maeneo hayo hususani wanaotumia usafiri wa majini, kupata taarifa
kwa ajili ya kujilinda na kuweka mikakati ipasavyo ili kuepuka maafa na matatizo yanayohusiana na hali ya hewa.
Tuna imani mamlaka inaendelea kushirikiana na wadau ikiwamo shirika lisilo la kiserikali la Uhifadhi wa Mazingira
na Maendeleo ya Kiuchumi (EMEDO) katika kutekeleza majukumu yake ya kutoa utabiri wa hali ya hewa kwa
manufaa ya jamii nzima ya Watanzania.
Maana hata taarifa ya Meneja Mradi wa Emedo, Arthur Mugema imeweka bayana kwamba ushirikiano kati yao na
TMA ndio umeleta matokeo ya kuandaa na kuweka kifaa hicho kwenye kisiwa cha Goziba ambacho kitaboresha
upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa kwenye maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria.