Uchaguzi AUC 2025: Kapt. Ibrahim, watano wengine kutoshiriki

Burkina Faso iliwahi pia kusimamishwa kwa muda mwaka 2015. Mataifa mengine ni Guinea, Gabon, Niger, Sudan na Mali.

ADDIS ABABA, Ethiopia — Kiongozi wa Burkina Faso, Kapt Ibrahim Traoré na viongozi wengine watano kutoka mataifa ya Afrika hawataungana na viongozi wa nchi na serikali wanaokutana leo na kesho Addis Ababa kwa ajili ya uchaguzi wa Mwenyekiti, Naibu na Makamishna wanane wa Umoja wa Afrika (AUC).

Wakati viongozi 49 akiwemo Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan wakiwa tayari mjini Addis Ababa kushiriki Mkutano wa kawaida wa 38 wa Wakuu wa Nchi na serikali wa Umoja wa Afrika (AU), mataifa 6 yanakubwa na vizuizi vya umoja huo.

Uchaguzi wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) umepangwa kufanyika Februari 15 na 16 macho yote yakielekezwa kwa wagombea watatu wa nafasi ya uenyekiti: Raila Odinga wa Kenya, Mahmoud Ali Youssouf wa Djibouti, na Richard Randriamandrato wa Madagascar. 

Advertisement

AU inajumuisha mataifa 55, yaliyogawanywa katika kanda tano za kijiografia zilizobainishwa na Umoja wa Nchi za Afrika mwaka 1976, zinazoakisi nchi zote za bara la Afrika.

Burkina Faso ilifungiwa ushiriki wake katika umoja huo mnamo Januari 2022 baada ya wanajeshi wakiongozwa na Ibrahim Traoré kumpindua rais aliyechaguliwa kidemokrasia.

Nchi hiyo iliwahi pia kusimamishwa kwa muda mfupi mwaka 2015.

Guinea, Burkina Faso, Sudan na Mali—ambayo ilifungiwa mapema mnamo 2021—ziliomba kusitishiwa vikwazo vyao mnamo Februari 2023, lakini maombi yao yalikataliwa.

PIA SOMA: Uchaguzi wa Uenyekiti wa AUC 2025: Mchuano mkali wa Kikanda

Katika kikao chake cha 1001 kilichofanyika Juni 1, 2021, Baraza la Amani na Usalama la AU liliazimia, kwa mujibu wa kanuni zake, kuisimamisha Mali kushiriki shughuli zote za AU hadi pale utawala wa kikatiba utakaporejeshwa.

Kwa sasa, Mali inaongozwa na Kanali Assimi Goïta kama Rais wa Serikali ya Mpito. Nchi hiyo ilifungiwa baada ya AU kulaani na kukataa vikali mapinduzi ya kijeshi na mabadiliko haramu ya serikali barani Afrika, kwa mujibu wa Kifungu cha 4(p) cha Mkataba wa AU. 

Mataifa mengine kama Sudan, ilifungiwa mnamo Oktoba 2021 baada ya Jenerali Abdel Fattah al-Burhan kutwaa madaraka kutoka kwa serikali ya mpito. Nchi hiyo haitashiriki katika uchaguzi hadi utawala wa kiraia utakaporejeshwa. 

Wakati Gabon ilifungiwa ushiriki wake baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea Agosti 2023, ambapo afisa wa kijeshi Brice Oligui Nguema alichukua madaraka. Nchi hiyo imeondolewa kwenye orodha ya wapiga kura katika uchaguzi huu. 

Niger ilifungiwa mnamo Agosti 2023 baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika Julai 2023. Rais Abdourahamane Tchiani alichukua madaraka kupitia Baraza la Kitaifa la Kulinda Taifa (CNSP), na hivyo kusababisha nchi hiyo kutoshiriki katika uchaguzi wa AUC.

Ili kuchaguliwa kama mwenyekiti wa AUC, mgombea lazima apate angalau theluthi mbili ya kura kutoka kwa Baraza la Wakuu wa Nchi na Serikali, ambalo linajumuisha wanachama 55 wa AU wanaomchagua na kumteua mwenyekiti na naibu mwenyekiti wakati wa Kikao cha Kawaida cha Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) huko Addis Ababa, Ethiopia.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *