MBUNGE wa Mkuranga, Abdallah Ulega amewahakikishia wananchi wa Mkuranga kwamba mwaka huu serikali itajenga madaraja matatu yaliyoainishwa kwa ujenzi kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni tatu.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara jana, Ulega ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi alisema kwamba serikali imetenga fedha hiyo ili jimbo la Mkuranga lifunguke kiuchumi.
Alisema kwamba serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha hizo kutekeleza ahadi yake ya kurahisisha usafiri na usafirishaji ili miradi ya maendeleo itekelezwe vizuri na kipato cha wananchi kiongezeke.
“Lengo la serikali ni kuunganisha jimbo letu la Mkuranga na maeneo mengine ili kuinua uchumi wa jimbo letu. Tukiweza kufanya biashara kwa urahisi jimbo letu kufunguka kiuchumi,” alieleza.
Alitaja madaraja yatakayojengwa kuwa ni litakalounganisha Shungubweni, Marogolo na Kongo Mulanzi. Daraja la Msolwa litakalounganisha Kisahani na Malela na Nguja Kilamba mpaka Tipo.
Alisema awali zilitengwa Sh milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja lakini kutokana na umuhimu wa miundombinu katika Jimbo la Mkuranga, Rais Samia ameongeza hadi ya Sh bilioni tatu kwa ajili ya maendeleo ya wilaya nzima ya Mkuranga.
Ulega alitoa rai kwa wajenzi wa madaraja hayo kuyajenga kwa wakati, ufanisi na kutumia fedha kwa nidhamu ili ubora wa madaraja uendane na thamani ya fedha iliyotolewa.
“Tujitahidi kutekeleza ujenzi kwa wakati na thamani ya fedha tuliyopewa ionekane. Tukiyatimiza haya itakuwa rahisi kupata fedha nyingine kutoka serikalini kwa ajili ya maendeleo ya jimbo letu,” alifafanua.