Umuhimu wa maboresho ya kodi kupitia ushirikishaji umma

KODI ni muhimu katika kufadhili shughuli za maendeleo ya kiuchumi na huduma za umma Afrika Mashariki.

Serikali za ukanda huu hutegemea mapato ya kodi kufadhili miundombinu, huduma za afya, elimu na hata programu mbalimbali za kijamii.

Hata hivyo licha ya umuhimu huo, maboresho ya sera za kodi hukumbana na changamoto kutokana na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoaminiwa katika umma, ukosefu wa ufahamu na ushiriki mdogo katika mchakato wa utungaji sera.

Advertisement

Katika nchi nyingi za Afrika Mashariki, wakati mwingine sera za kodi huchukuliwa kama hatua zilizowekwa na
serikali, badala ya mifumo iliyobuniwa kwa ushirikiano unaoakisi mahitaji ya watu.

Kihistoria hali ya uwepo wa mawasiliano duni kati ya watunga sera na wananchi pamoja na kukosekana kwa uwazi ni miongoni mwa mambo yanayochangia usimamizi wa kodi kutofanikiwa, kuwapo viwango vya chini vya utekelezaji wa kanuni nasheria za kodi (ulipaji kodi) pamoja na kuongezeka kwa ukwepaji kodi.

Biashara nyingi na hata watu binafsi hasa katika sekta isiyo rasmi hujihisi kutengwa katika maboresho ya kodi hali inayosababisha kuwapo changamoto zaidi katika utekelezaji. Ili kushughulikia suala hili na kuchochea ushiriki wa jamii katika kutunga sera ya kodi, ni muhimu kujenga mifumo ya kodi ambayo ni ya haki, endelevu na yenye ufanisi.

Kwa wananchi, wafanyabiashara na taasisi za kiraia kushirikishwa kikamilifu, serikali za Afrika Mashariki zitajenga uaminifu, kuzitaboresha ulipaji kodi na zitabuni sera zinazoakisi hali halisi ya kiuchumi. Kutumia mbinu hii
shirikishi kunatoa uhakika kuwa, maboresho ya kodi si tu kwamba yanakubalika kitaal amu, bali pia yanathibitishwa
kidemokrasia.

Katika makala haya tutaangalia kwa undani umuhimu wa ushiriki wa umma katika kuundaji sera ya kodi, mikakati ya ushiriki iliyopo, shuhuda za mafanikio kutoka katika kanda hii ya Afrika Mashariki na njia za kuboresha ushiriki wa jamii katika uundaji wa mifumo ya kodi Afrika Mashariki.

Aidha, yataangalia mikakati ya ushirikishwaji wa umma iliyopo, mafanikio na changamoto zake pamoja na mambo
ya kujifunza kutokana na tafiti zinazingatia ushiriki kamilifu wa raia katika uundaji wa sera ya kodi. Uchambuzi unatokana na tafiti za maoni ya umma na ripoti za mipango ya awali ya ushiriki. Kwa kawaida, serikali na mamlaka za kodi hutumia mbinu mbalimbali kushirikisha wananchi katika mijadala kuhusu sera ya kodi.

Jambo hili linasisitizwa na Suzanne Diu kutoka Kundi la Emirate (Emirates Group) anayesema majadiliano na usikilizaji umma hutoa majukwaa muhimu kwa watu binafsi, biashara na mashirika ya kiraia kutoa mrejesho wa
maoni kuhusu sera za kodi zinazopendekezwa.

Anasisitiza kuwa, mazungumzo hayo yanapaswa kuwa endelevu na yanayobadilika badala ya kuwa matukio ya mara moja. Tafiti pamoja na kura za maoni nazo zina umuhimu wa kipekee kwani husaidia watunga sera kupima uelewa wa umma na mitazamo yao kuhusu kodi na hivyo, kubainisha maeneo yanayohitaji ufafanuzi zaidi au marekebisho.

Mtendaji mwandamizi katika benki inayoongoza nchini Uganda, James Raphael anasisitiza umuhimu wa kufanya kampeni kupitia vyombo mbalimbali vya habari kama redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii kusambaza taarifa zinazohusu kodi na kuhimiza ushiriki wa umma katika maboresho yanayoendelea.

Kwa mtazamo wake, ushirikishwaji uliopo kupitia njia hizi kwa sasa ni mdogo jambo linaloweza kuwa linazuia uwezo wa tume kukusanya mtazamo bora kutoka kwa wadau hasa wa ngazi ya chini.

Hata hivyo, anadokeza kuwa, Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi inaweza kuwa ilitarajia changamoto hii na kutaka kuishughulikia kwa kutumia machapisho yanayosambazwa sana kama vile magazeti ya Daily News Toleo la Afrika Mashariki, HabariLEO Afrika Mashariki na majukwaa ya magazeti hayo.

Kwa kuwezesha mijadala mipana zaidi na kujumuisha maoni mbalimbali, mkakati huu utahakikisha kunakuwapo
mazungumzo jumuishi zaidi kuhusu sera ya kodi hadi nje ya mipaka ya Tanzania ili kushirikisha wadau katika eneo zima.

Mbali na matumizi ya vyombo vya habari katika suala hili, utafiti unaonesha kuwa baadhi ya nchi zimepitisha mbinu zilizopangwa zaidi za ushirikishwaji wa umma. Kamati za ushirikishwaji wa wadau zinazojumuisha wawakilishi kutoka sekta binafsi, vyama vya wafanyakazi na mashirika ya utetezi yana nafasi muhimu katika uundaji wa sera za kodi kwa kutoa maoni.

Kimsingi, majadiliano kati ya umma na sekta kibinafsi hutumika kama majukwaa muhimu ya moja kwa moja ya
majadiliano kati ya mamlaka ya kodi na viongozi wa biashara, kusaidia kuhakikisha kwamba kanuni za kodi
zinazoendana na hali halisi ya kiuchumi na changamoto mahususi kisekta.

Changamoto
Pamoja na Tume kupata maendeleo yanayostahili pongezi, lazima changamoto kadhaa zishughulikiwe katika ripoti yake ya mwisho kwa Rais ili kuhakikisha kuna ushiriki wa kutosha wa umma katika utungaji wa sera ya kodi.

Mmoja wa wafanyakazi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Idara ya Afrika anayekataa kutajwa jina anasema kati ya masuala muhimu zaidi ni uelewa mdogo wa umma na kuhusu sera za kodi miongoni mwa Watanzania.

Anasema ukosefu huu wa uelewa unaweka ugumu kwa wananchi wengi kuchangia katika vikao vya majadiliano.
Anasema matokeo ya hali hii mara nyingi ni kurudia malalamiko yanayofahamika au kugeukia mada zisizohusiana, badala ya kutoa maoni ya kujenga kuhusu maboresho ya kodi.

Mbali na upungufu huu katika maarifa, imani ya umma kwa taasisi za serikali bado ni changamoto kuu.

Kwa mujibu wa uzoefu wa kihistoria, rushwa na usimamizi mbaya ni miongoni mwa mambo yanayokatisha tamaa
wananchi wengi na kuwafanya wengine wasishiriki mijadala kuhusu kodi. Kimsingi, hata sekta isiyo rasmi ambayo ni sehemu kubwa ya uchumi wa nchi inakabiliwa na kutoshirikishwa katika mazungumzo na mijadala hii.

Wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi wanapowakilishwa, masuala yao huchukuliwa kwa uzito mdogo au maneno ya kisiasa na hata kwa maelezo ya kiitikadi bila kushughulikia hali halisi inayowakabili. Vikwazo vya kimawasiliano
navyo huzidisha ugumu wa mchakato.

Juhudi nyingi za ushirikishwaji hufanywa kadiri ya taratibu za urasimu ambazo kimsingi, hazifikii wananchi wa kawaida hususani wa vijijini. Kwa mfano, mtu anajiuliza ni wakulima wangapi, wavuvi wangapi au hata vibarua wangapi kutoka maeneo ya mbali huhusika moja kwa moja katika mchakato huu?

Hali ya Tume kutegemea mbinu ngumu za mtandaoni kama nyenzo ya msingi kwa ajili ya maoni ya umma, inaweka uwezekano mkubwa kuwa imetenga kundi kubwa la watu wasio na nyenzo au wasio na uelewa wa mifumo kama hiyo.

Mbali na hayo, hata ushirikishwaji umma unapofanyika, mara nyingi hakuna njia za ufuatiliaji zilizo wazi kuonesha
michango ya wananchi inavyoathiri uamuzi wa mwisho wa kodi. Kukosefu huku kwa uwazi huchochea mkanganyikio na kutoshirikishwa na hatimaye kudhoofisha uhalali wa mchakato wa maboresho ili kutatua changamoto hizi.

Jambo hili lazima liwe kipaumbele cha Tume hii inapokamilisha ripoti yake kwa Rais. Kimsingi, bila kuwapo juhudi za makusudi kuimarisha ufikiaji/upatikanaji, ushirikishwaji na uwajibikaji katika mchakato wa ushiriki,
maboresho ya kodi yataonekana katika hatari ya kuwa kama yaliyotengwa na hali halisi ya watu hasa wanaokusudiwa kuwahudumia.

Mapitio ya mifano
Ili kuonesha changamoto za ushiriki wa umma katika utungaji sera ya kodi, makala yanajikita katika tafiti tatu
muhimu kutoka Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Mifano hii inasisitiza masuala kama vile uelewa mdogo wa watu, ukosefu wa imani kwa taasisi za serikali,
kutoshirikishwa kwa sekta isiyo rasmi, vikwazo vya mawasiliano na kukosekana kwa taratibu za ufuatiliaji.

Anguko la Tanzania mwaka 2016
Mtafiti wa kujitegemea kutoka Taasisi ya Usimamizi wa Kodi Tanzania iliyopo Dar es Salaam, Jumanne Msuya
anajikita katika mabadiliko makubwa ya kisera ya mwaka 2016 Tanzania ilipoanzisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika pembejeo za kilimo kama vile mbegu, mbolea na viuatilifu.

Hatua hii iliibua ukosoaji mkubwa kutoka kwa wakulima waliodai kodi hiyo ingeongeza gharama za uzalishaji na kuhatarisha usalama wa chakula.

Kwa mujibu wa Msuya, wakulima wengi wadogo hawakushirikishwa moja kwa moja wakati wa mchakato wa kuandaa sera badala yake, wasiwasi wao ulioneshwa kwa kiasi kikubwa na wanasiasa badala ya wawakilishi wa sekta husika wenye utaalamu katika kilimo.

Matokeo yake, sera hiyo ilishindwa kubaini changamoto halisi zinazowakabili wakulima vijijini na hivyo, kusababisha watu wengi kutoridhika.

Ili kukabiliana na upinzani ulioongezeka, mwaka 2017 serikali ililazimika kubatilisha uamuzi huo na hatimaye
kutoza kodi ya pembejeo za kilimo. Mfano huu unaonesha wazi hatari za kupuuza ushiriki wa moja kwa moja wa wananchi na vikundi vinavyoathirika, hasa jamii za watu walio vijijini.

Kukosekana kwa mashauriano jumuishi husababisha kushindwa kwa sera na kuilazimu serikali kurudi nyuma.
Kimsingi, mfano huu unatumika kama ukumbusho muhimu kuhakikisha sera za kodi zinaonesha hali halisi ya
idadi ya watu inayoathirika.

Tatizo la Uganda mwaka 2018
Julai 2018, Uganda ilianzisha kodi ya kila siku kwa matumizi ya mitandao ya kijamii ikilenga kuongeza mapato ya serikali na kudhibiti mawasiliano ya mtandaoni.

Kwa mujibu wa mtafiti katika Chuo Kikuu cha Makerere, Namazzi Byaruhanga, sera hiyo ilikabiliwa na upinzani mkubwa hasa kutoka kwa vijana, wajasiriamali wa kidijiti (mtandaoni) pamoja na mashirika ya kiraia nchini humo.

Mojawapo ya shutuma kuu ilikuwa kutokuwapo mashauriano ya umma kabla ya utekelezaji wa kodi hiyo. Byaruhanga anasisitiza kuwa, Waganda wengi hasa wa vijijini hawakuwa wanajua lolote kuhusu kodi hiyo hadi
walipoona makato kwenye akaunti zao za simu.

Anasema ukosefu huu wa mawasiliano ulizua mkanganyiko hasa katika jamii zilizo pembezoni zilizoathiriwa zaidi na sera hiyo. Kwa kiasi kikubwa, mchakato wa ushiriki ulitegemea mikutano yenye urasimu iliyofanyika maeneo ya mijini bila kuhusisha sauti za wananchi wa vijijini na wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi wanaotegemea zaidi  mitandao ya kijamii kwa mawasiliano na biashara.

Kutojumuisha mitazamo tofauti kulisababisha maandamano makubwa, huku Waganda wakihoji kuhusu haki na uwazi katika kodi. Kilio cha wananchi hususani vijana, kilichangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa matumizi ya mitandao ya kijamii, hivyo kudhoofisha lengo kuu la kupata mapato zaidi.

Kutokana na hali hiyo, utekelezaji wa kodi hiyo haukufikia matarajio ya mapato zaidi na badala yake, ulibainisha haja kubwa ya kuwapo mchakato wa mashauriano ya umma ambao ni jumuishi zaidi na unaoweza kufikiwa wakati
wa kutunga sera zinazoathiri idadi ya watu wote.

Nchini Kenya mwaka 2020 Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Karatina, Kampasi ya Riverbank, John Peter anatoa data
muhimu zinazotoa mwanga kuhusu uanzishwaji wa kodi ya huduma za kidijiti wa mwaka 2020 uliolenga kuongeza
mapato kutokana na ukuaji wa uchumi mtandaoni.

Kwa mujibu wa utafiti wake, licha ya juhudi za serikali kufanya mijadala ya umma, wajasiriamali wengi wadogo wa kidijiti hasa walio katika sekta isiyo rasmi hawakuwa na taarifa kuhusu mijadala hii. Peter anasema uchunguzi
uliofanywa na Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA) ulibaini kuwa, takribani asilimia 60 ya waliohojiwa hawakuwa
wamesikia kuhusu kodi hiyo hadi ilipoanza kutekelezwa.

Kwa kiasi kikubwa, mchakato wa mashauriano uliegemea kwenye vyama vilivyo katika sekta rasmi na mawasilisho ya mtandaoni yaliyoacha wadau wengi wa chini wakikokosa njia za kuwawezesha kushiriki. Pengo hili lilisababisha
msukosuko mkubwa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa kidijiti waliohisi sera iliundwa bila mchango wao au kwamba iliundwa bila kuzingatia changamoto zao.

Upinzani huo ulioenea zaidi hasa kutoka sekta ya teknolojia, uliilazimisha Serikali ya Kenya kurejea na kurekebisha vipengele fulani vya kodi ya huduma za kidijiti ikisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa umma katika utungaji sera.

Mfano huu unaonesha namna ushirikishwaji duni kwa wadau wakuu hususani walio katika sekta isiyo rasmi,
unavyoweza kusababisha mkanganyiko, watu kutoridhika na hatimaye kuchochea kuwapo hitaji la marekebisho ya sera.

Unahimiza ulazima wa serikali kutumia zaidi mbinu za mashauriano jumuishi na zinazoweza kufikiwa ili kuepuka kutenga sehemu muhimu za uchumi hasa sekta za kidijiti hususani zinavyoendelea kukua na kubadilika.

Kifuatacho
Akitoa maoni yake hivi karibuni, mmoja wa wanachama waandamizi wa chama kikuu cha upinzani nchini, anasema ili kuimarisha ushiriki wa umma katika utungaji wa sera ya kodi, serikali inapaswa kurahisisha mawasiliano kwa kuwasilisha sera za kodi kwa lugha ya wazi na isiyo ya kitaalamu inayosaidiwa na vielelezo vya picha.

Profesa mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anaunga mkono hisia hizo akisisitiza umuhimu wa kupanua ushirikiano wa kidijiti kupitia mitandao ya kijamii, programu tumizi za simu na tafiti za mtandaoni ili
kufikia hadhira kubwa zaidi hasa vijana.

Anasisitiza umuhimu wa kutumia majukwaa yanayofikika na kuepuka matumizi ya mifumo migumu. Wakuu wa wilaya nchini pia wanahimiza umuhimu wa kushirikisha jamii kupitia ushirikiano baina ya taasisi ndogo na viongozi wa jamii.

Wanasema njia hii itasaidia kuongeza uelewa kuhusu kodi na kuhakikisha taarifa zinapatikana kwa watu katika maeneo ya mikoa mbalimbali. Mmoja wa wakuu wa wilaya anasema uhamasishaji huo unapaswa kuwa kipaumbele
katika ukusanyaji maoni ya wananchi hasa katika masuala yanayoathiri taifa kwa ujumla.

Akirejea ujumbe wa Rais Samia Suluhu Hassan, mkuu wa wilaya huyo anasema, “Taifa hili si la watu waliobahatika kuwu wasomi pekee, bali ni la kila mtu.” Lingine muhimu lililobainishwa na mfanyakazi mwingine wa IMF na kuungwa mkono na mchumi mwanadamizi katika Benki ya Dunia, ni umuhimu wa kuanzisha na kuendeleza
utaratibu wa kutoa maoni.

Mfumo huu utaruhusu wananchi kuona namna michango yao inavyounda sera za kodi na hivyo kuchochea hisia za
umiliki na kujihusisha katika mchakato.

Ilikubaliwa pia kuwa, kuimarisha uwakilishi tofauti katika mijadala ya sera ya kodi kwa kujumuisha wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi, wafanyabiashara wadogo na makundi yaliyo pembezoni kutachangia kuwapo mfumo wa kodi ambao ni jumuishi na wenye usawa zaidi.

Washiriki wengi wanasisitiza umuhimu wa kukagua na kufanya mapitio katika matumizi ya serikali na changamoto
zinazohusiana nazo. Wanasema uelewa wa kina wa vipengele hivi ni muhimu kwa maboresho ya kodi yenye ufanisi.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *