Utashi kisiasa utachagiza ukuaji wa uchumi Tanzania, Namibia

TANZANIA juzi imempokea Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah aliyefika nchini kwa ziara ya kikazi kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais wa nchi hiyo.
Ujio wake nchini umebeba dhana ya kuimarisha ushirikiano wa kindugu na kiuchumi baina ya Tanzania na Namibia na uhusiano ulioasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Baba wa Taifa la Namibia, Sam Nujoma.
Mchango wa Tanzania kwa uhuru wa Namibia uliopatikana mwaka 1990 hakuna asiyeufahamu kwani Netumbo aliishi Magomeni, Dar es Salaam na viongozi wengine nchini katika harakati hizo.
Rais Samia Suluhu Hassan na Netumbo wamekubaliana kuuondoa umasikini na kukuza uchumi endelevu wa nchi wanazoziongoza. Maeneo waliyokubaliana juzi ni pamoja na eneo la biashara.
Kwa mujibu wa Rais Samia, kiwango cha biashara kati ya Namibia na Tanzania kimepanda kutoka Sh bilioni 17 hadi Sh bilioni 20 kati ya mwaka 2019 hadi 2023 lakini anaamini kuna fursa kubwa ya kufanya vizuri zaidi.
Kutokana na hilo, Rais Samia amewaalika wafanyabiashara wa Namibia kuja kuwekeza nchini na kuwakaribisha kushiriki katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba mwaka huu ili kushirikiana na wenzao wa Tanzania kukuza biashara.
Maeneo mengine ya ushirikiano ni mafuta na gesi ambayo nchi zote zina rasilimali hizo na tayari Namibia wameanza kupata mafuta. Zipo pia sekta za mifugo, uvuvi, kilimo na mazao yake, madini, utalii, uchumi wa buluu na utamaduni.
Tunaamini ushirikiano huu utaongeza fursa za kiuchumi za kikanda katika kuhamasisha soko huru la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Soko Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Kuhusu Kiswahili, kama ilivyoelezwa kwamba tayari Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa kushirikiana na chuo kingine cha Namibia wamekubaliana kuanza kufundisha Kiswahili ngazi ya chuo, ni imani yetu mafanikio yake yatakuwa makubwa kwani vijana wa Kitanzania na Kinamibia watapata ajira.
Tunaamini uzoefu wa Namibia katika sekta hizo hasa ya uchumi wa buluu utaongeza kasi ya ongezeko la ajira kwa wananchi wa mataifa hayo.
Utashi wa kisiasa kwa viongozi hao wawili wanawake shupavu Afrika ni dhahiri, hivyo wakipata wasaidizi na watendaji makini, dhamira na nia yao njema kuleta ukombozi wa kiuchumi kwa nchi zao utatimia.
Tunaamini ni wakati muafaka wa kuwaunga mkono katika haya ili rasilimali za mataifa haya ziwanufaishe kwanza wananchi.
Very interesting read—easy to understand and packed with useful info!