KUELEKEA siku ya mazingira duniani Shirika lisilo la Kiserikali la ‘Mazingira ni Uhai’ (ENLIFE) limepanda nyasi 1200, eneo la Kibwegere jijini Dar es Salaam, ili kuzuia mmomoyoko wa ardhi na uharibifu wa mazingira.
Akishiriki katika tukio hilo Balozi wa Mazingira kutoka ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Godfrey Mwimanzi amesema jambo la kutunza mazingira linapaswa kutiliwa mkazo na watu wote.
“Tunapaswa sote kutunza mazingira kwani kunapotokea mabadiliko ya tabianchi waathirika ni watu wote bila kujali itikadi au tofuati za kidini, kabila au rangi,” amesema Mwimanzi.
Amesema ni vyema kila mtu popote alipo atunze mazingira na awe balozi wa kupanda miti ili dunia iwe mahali salama pa kuishi.
Mwimanzi amesema kutokana na uharibifu wa mazingira, nchi imekuwa na ukame uliosababisha vyakula vimepanda bei hivyo amewasihi Watanzania kutunza mazingira kwa kupanda miti na kutokata miti hovyo.
“Paroko amezungumzia anasikitika anapopita barabarani anaona pikipiki zimesheheni magunia ya mikaa, maana yake miti yetu inateketea. Miti inalia ijapokua haiongei,” amesema Mwimanzi na kuongeza:
“Leo ENLIFE wamekuja kupanda nyasi na miti kuzuia maporomoko ya udongo pamoja na athari za vyanzo vya maji .”
Naye Paroko wa Parokia ya Mt. Theresia wa Avila Kibwegere, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Evodius Nachenga amesema elimu zaidi ya mazingira inapaswa kutolewa, ili kila Mtanzania aweze kuona thamani ya kupanda miti ikiwa ni pamoja na kutunza mazingira.
Paroko ametoa wito kwa serikali kugawa vitalu kwa wakata mikaa, ili wapande miti na waitunze kwa ajili ya biashara hiyo, kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kupunguza uharibifu wa mazingira na kuweza kutunza vyanzo vya maji.
“Naumia sana ninapokutana na pikipiki zimebeba mikaa maana yake hapo mti umekufa. Ni vyema kuwepo na utaratibu wa watu kupanda miti kuitunza na hatimaye itumike kwa manufaa yao na kwa taifa kwa ujumla,” amesema Paroko Nachenga.
Naye Mratibu wa ENLIFE Tanzania, Gerald Muunga amesema wametambulisha rasmi nyasi aina ya ‘vetiver’ ambao una uwezo wa kuhifadhi maji na udongo kuimarisha ardhi kuboresha maji na kudhibiti uchafuzi na kuweza kupunguza ukali wa maafa.
“Teknolojia hii inatumika katika mabara mbalimbali duniani, ikiwemo Tanzania kwa uchache sana. Hivyo sisi tumeamua kuihuisha kwa kubuni mradi huu, baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya madaraja, makaburi, yanazolewa kutokana na mmomonyoko, kingo za mito na barabara zinabomoka, rutuba kwenye ardhi inazidi kupotea,” amesema Muunga.
Amesema ENLIFE itaendelea kutoa elimu sambamba na kupanda nyasi katika harakati za kuunga mkono utunzaji wa mazingira na kauli mbiu ya tusome na Muunga alisema kwa sasa wanahusisha sana watoto wanafunzi kuanzia chekechea na shule za msingi.
“Kauli mbiu yetu ya mwaka huu ni Mti kwa kila mtoto kupanda mti ni ishara ya matumaini ya baadaye na watoto wanahitaji kuwa na matumaini sasa na zaidi na hata milele,” amesema Muunga.
ENLIFE imeshirikiana na serikali ya mitaa, Mtaa wa Kibwegere pamoja na Kanisa Katoliki Parokia ya Kibwegere.