Viongozi serikali za mitaa wafundwa Bukombe

VIONGOZI wa serikali za mitaa, halmashauri ya wilaya ya Bukombe mkoani Geita wamesisitizwa kuwekeza kwenye mfumo shirikishi wa kijamii katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo na utatuzi wa kero za wananchi.

Maelekezo hayo yametolewa katika semina iliyoratibiwa na Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Rais Tamisemi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Kituo cha Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Mkaguzi wa Hesabu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, Hamis Mjanja amesema maelekezo hayo ni sehemu ya mafunzo maalum ya uraia na utawala bora yanayolenga kuongeza weledi, uwajibikaji na utendaji kwa viongozi wote.

Advertisement

Amesema mfumo shirikishi kwa viongozi wa serikali za mitaa utasaidia kutatua kero mbalimbali za wananchi katika hatua za awali pasipo kutegemea viongozi wa juu na kutoa fursa ya wananchi kushiriki kwenye miradi ya maendeleo.

Amesema pia kupitia mafunzo hayo yaliyojumuisha viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Watendaji wa Kata na Wakuu wa Idara ipo haja ya kuweka mipango thabiti ya kuimarisha ulinzi na usalama nchini.

“Tunajua Bukombe inapakana na mkoa wa Kigoma ambao unapakana na nchi jirani ambazo usalama wake siyo rafiki kwa hiyo mikakati wanayoweka Kigoma wakishirikiana na Bukombe itasaidia sana”, amesema Mjanja.

Mratibu wa Mafunzo ambaye ni wakili kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Joyce Mushi amesema mafunzo hayo yamewalenga viongozi wa serikali za mitaa kwani ndio watu wa mwanzo kukutana na wananchi.

“Haya yameletwa kwetu kwa sababu sisi tunakutana na wananchi moja kwa moja, kwa kipindi hiki sisi tumepanda mbegu ambayo itaenda vijijini ili wananchi nao waweze kupata elimu hii”, amesema Joyce.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Bukombe, Pasikasi Mulagiri amewataka wanufaika wa mafunzo hayo kuyapokea na kuimarisha utendaji wao badala ya kuendelea kufanya kazi kwa mazoea kwenye maeneo yao.

Mulagiri amekiri ipo changamoto ya miradi mingi kutokamilika kwa wakati kutokana ushirikiano hafifu wa viongozi katika usimamiaji wa miradi hiyo.

“Watendaji ndio viungo wa serikali na wananchi kule chini, na jambo la utawala bora ni jambo ambalo linatuhusu sisi wote kwani bila kuwa na utawala bora suala la haki, wajibu, hayawezi kufanikiwa”, amesema Mulagiri.

Ofisa Mtendaji Kata ya Bugelenga wilayani humo, Dora Juma amesema mafunzo hayo yamezikumbusha taasisi, idara, na vitengo vyote ndani ya halmashauri kufanya kazi kwa ushirikiano ili kupunguza kero za kijamii.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *