Vitega uchumi vya Dodoma City, Mtumba kuanza kazi Novemba

Vitega uchumi vya Dodoma City, Mtumba kuanza kazi Novemba

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru amesema vitega uchumi vya Hoteli ya Dodoma City na kile cha Mtumba vinatarajia kuanza kufanya kazi Novemba Mosi mwaka huu.

Pia amesema Halmashauri ya Jiji ina mpango wa kupeleka asilimia kubwa ya mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa wafanyabiashara waliohamishiwa kwenye soko la wazi la Machinga.

Mafuru ameyasema hayo jijini hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na maendeleo ya miradi inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Advertisement

Alisema hatua hiyo inatokana na kukamilika kwa zabuni za kuwapata watoa huduma kwa vitega uchumi hivyo.

“Kwa upande wa mradi wa Dodoma City Hoteli imekamilika kwa asilimia 100 na taratibu za manunuzi pia imekamilika na tumeshampata mtoa huduma ambaye kwa sasa anafanya marekebisho. Mpaka sasa ameshaingiza zaidi ya shilingi milioni 300 kwa marekebisho anayoyataka,” alisema.

Kuhusu kitega uchumi cha hoteli ya kisasa na kumbi za mikutano kilichojengwa katika mji wa serikali, Mafuru alisema taratibu za manunuzi zimekamilika baada ya kumpata mtoa huduma huku ofisi zikiwa zimepata wawekezaji.

Aidha, Mafuru alisema asilimia kubwa ya mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma yataelekezwa kwa wafanyabiashara wa soko la wazi la machinga ambao kwa sababu watakuwa wanatambulika kwa eneo wanalofanyia kazi na taarifa zao zimehifadhiwa.

Alisema kwa sasa tayari Halmashauri ya Jiji la Dodoma limetenga Sh bilioni tano kwa ajili ya kuwakopesha wafanyabiashara wadogo na asilimia kubwa itaelekezwa kwa wamachinga wa soko la kisasa ili waweze kuinua mitaji yao.

 

 

 

 

 

/* */