Vyama vitangulize amani kuliko madaraka

MWAKA 1992 chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere Tanzania iliingia tena katika mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Miongoni mwa vyama vya siasa vilivyoanzishwa katika mfumo huu vyenye usajili wa kudumu ni pamoja na NCCR Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichokuwapo tangu mwaka 1977.
Vingine kwa mujibu wa tovuti ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni UMD, NLD, UPDP, NRA, ADATADEA), TLP, UDP, Demokrasia Makini DP, SAU, AAFP, Chama Cha Kijamii (CCK) na ACT-Wazalendo.
Mfumo huo uliikuta nchi ikiwa katika amani na utulivu na viongozi wote waliopita katika uchaguzi wowote katika mfumo huo wamehakikisha wanalinda na kutunza tunu ya amani Tanzania ambayo inapaswa kuendelezwa.
Kwa mtazamo wangu, ninayoyasikia na kuyaona kupitia vyombo vya habari katika nchi nyingine zilizotumbukia katika machafuko na kupoteza amani na utulivu, yanatoa funzo kuwa ni rahisi kupoteza amani, lakini kuirejesha ni ‘mtihani mgumu.’
Somo lingine ni ukweli kuwa, chanzo kikubwa cha machafuko au mapigano katika nchi nyingi duniani zikiwamo za Afrika, ni baadhi ya vyama vya siasa kuogopa uchaguzi na kukataa matokeo huku vingine vikiogopa au kukiuka ‘mazungumzo ya mezani’.

Mfano mzuri ni machafuko ya hivi karibuni nchini Msumbiji yanayohusishwa na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 9, mwaka jana uliompa madaraka aliyekuwa mgombea wa Chama tawala cha Frelimo, Daniel Chapo na baadhi ya wananchi kutokubali sauti ya wapigakura hivyo, kuamua kuandamana kupinga ushindi huo.
Nchini Kenya baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2022 uliomtangaza mgombea wa Chama cha UDA, William Ruto kuwa mshindi dhidi ya mpinzani wake mkuu, Raila Odinga, kuliibuka machafuko yaliyosababisha watu kadhaa kupoteza maisha.
Si Kenya na Msumbiji tu, bali wapo waafrika wengine wanaomwaga damu za wenyewe kwa wenyewe kama Sudan na Sudan Kusini, mambo ambayo ni hatari kwa ustawi wao wenyewe.
Ndiyo maana nasema kwa mtazamo wangu, machafuko katika nchi nyingi husababishwa na ushawishi wa baadhi ya viongozi wa kisiasa wasiokubali kushindwa wakidhani uchaguzi bora, ni ule ambao wao ndio washindi huku wengine wakitaka waingie madarakani kwa kutumia ‘mabavu.’
Pia, viongozi wa vyama vya siasa wanabeba sehemu muhimu katika hatma ya amani na utulivu wa nchi, hivyo wanapaswa kuongozwa na kuenenda kwa hekima zinazozingatia ukweli kuwa siasa ni kwa ajili ya watu na si watu kwa ajili ya siasa.
Waongozwe na Roho wa Mungu juu ya busara zao ili badala ya kufanya mambo yanayoweza kuharibu amani ya nchi, wawe mawakili wa utetezi na askari wa ulinzi wa amani ya nchi kabla ya chochote mbele yao. Kwa msingi huo, watumie nguvu kubwa kuzuia na kuepusha uvunjifu wa amani nchini ili watu wafanye shughuli za maendeleo.
Wanachoweza kufanya wanasiasa ili wasiwe chanzo cha uvunjifu wa amani, ni kila mmoja kuhubiri amani
na maridhiano yanayokwenda pamoja na uvumilivu wa kisiasa.
Tanzania inapoelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani 2025, kila chama na kila mwanasiasa ama awe mwanachama au kiongozi, afanye siasa za kistaarabu zinazolenga kutoa majawabu kuhusu vikwazo au kero za wananchi na namna ya kupambamba navyo kuwapa watu maendeleo.
Wakati wa kampeni ukifika, kila mmoja afanye kampeni na siasa za kistaarabu, si siasa chafu za matusi, kashfa, vitisho na utitiri wa malalamiko unaosaka huruma za watu na wadau wa kimataifa.

Wanasiasa na viongozi wao katika vyama vyote wafungue milango ya masikio na akili zao kupokea mahubiri ya viongozi wa dini ambao wana wajibu wa kufanya ‘doria za kiroho’ hata kwa wanasiasa maana wote ni ‘abiria wao’. Wananchi wakumbushwe kuwa mihemko ya kisiasa haina tija badala yake, hutimiza msemo kuwa ‘mchuma janga hula na wa kwao.’
Kwamba, machafuko yatakapotokea kama si mwanasiasa mwenyewe hudhurika kwa namna moja ama nyingine, wengine watakaotumbukia katika shimo la mateso ni watoto, mama, wake, waume, ndugu, jamaa au rafiki zao.
Hii inamaanisha kuwa, kuhubiri au kuendesha siasa zenye sura ya chuki kabla, wakati na hata baada ya chaguzi ni kufanya kosa la kuchimba shimo ili watumbukie wengine, kisha ukatumbukia mwenyewe.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufunuo, Paul Bendera anasema Watanzania wanaojificha kwenye mgongo wa siasa wakiwa ‘wamemezeshwa sumu’ na watu wenye malengo na masilahi binafsi, ‘wageuke na kutazama’ nchi zilizofanya kosa la ‘kugawa, kuuza au kuua amani’.
Kisha, watu hao waone nchi hizo namna zinavyoteseka huku wengine waliohusika kuchochea wakikiri kuwa majuto ni mjukuu ambaye huja kinyume cha matarajio.
Kimsingi, kupoteza ndugu, kupata ulemavu au majeraha na kulazimisha nduguzo kukuuguza na kusababisha umasikini nyumbani au kuifanya familia na ndugu zako kuwa wakimbizi kama matunda ya siasa za majitaka, ni kupiga ngumi ukuta huku ukijua unaumiza mkono wako.
Ndiyo maana, Askofu Bendera anataka watu wapate picha kutoka mataifa yaliyotumbukia kwenye shimo la machafuko kutokana na mambo ya siasa hasa uchaguzi mkuu kama kioo cha kujitazama na kutafakari wanatoka wapi, wako wapi na wanakwenda wapi.

Wawatazame wanaoathirika namna wanavyotafuta amani lakini hawaipati maana kama ilivyo kwamba ng’ombe hajui umuhimu wa mkia wake hadi unapokatika, ndivyo ilivyo kwamba baadhi ya watu hawajui thamani ya amani hadi inapopotea.
Askofu Bendera anasema, “Mtu apate picha ya mataifa jirani yenye machafuko na watu wajifunze. Mfano mzuri ni kwa jirani zetu Kenya… Waangalie watu wangapi wamepoteza maisha kutokana na machafuko nchini humo.”
Anaongeza: “Haiwezekani nchi iingie kwenye machafuko kwa ajili ya kutetea ‘ulaji’ na masilahi ya mtu mmoja…”
Anaongeza: “Kwa mfano, mimi nina miaka 60, hivi ‘kikinuka’ hapa nitaweza kukimbia! Siwezi, nitafia njiani. Sasa kwa nini nife kwa ajili ya mtu kutaka kufanikisha malengo yake binafsi.
“Tuache kutoa maneno ya chuki yanayochochea machafuko. Hivi tunadhani tu kimwaga damu, ni damu ya nani itamwagika kama si yetu wenyewe, watoto wetu, wazazi wetu na ndugu zetu wenyewe!” Anasema anachukizwa na matamko ya baadhi ya viongozi wa dini yanayounga mkono baadhi ya mambo haya hasa ya vyama vya siasa vinavyotaka kuvuruga amani nchini.
“Tuache kutoa matamko kwa mihemko, tuangalie na kupima madhara ya matamko tunayotoa hasa katika kipindi hiki tunachojiandaa kwa uchaguzi mkuu,” anasema kiongozi huyo wa kiroho. Mdau wa masuala ya siasa, Noel Rwekiza mkazi wa Tabora, anasema haoni haja ya vyama vya siasa kuchezea tunu ya amani ambayo ni zawadi ya Mungu kwa Watanzania.
“Wajue tu amani yetu ina thamani kubwa sana kuliko kitu chochote, waangalie nchi kama Congo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC) namna watu wanavyohangaika kukimbilia katika nchi nyingine. “Amani ni tunu, haifananishwi na vyeo au kitu chochote hivyo chondechonde Watanzania tusikubali kufikishwa huko,” anasema.
Rwekiza anasema baadhi ya wanasiasa wanaweza kutorosha familia zao kwenda nchi zenye amani na hata wao wenyewe wanaweza kuishi huko wakiwa wameacha ‘moto unaunguza’ wasio na hatia.
Jambo hili halikubaliki. “Kwa kweli wafanye vyote watuachie amani yetu na utulivu; wasitufikishe huko eti kwa kuwa wanataka waingie ikulu na hata hiyo ikulu ukiingia wakati umeleta laana sijui kama uongozi wako utakuwa na amani.”
Naye mkazi wa Ubungo, Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina la Matha Julius anawakumbusha watu kadhia ya mabomu ya Gongo la Mboto na Mbagala miaka kadhaa iliyopita jinsi ilivyotaabisha wanawake na watoto na kuwataka watu wakumbuke hayo kabla ya kuanzisha vurugu.
“Watanzania hasa wanawake wakumbuke hali ya taharuki na mateso yaliyotokea wakati wa milipuko ya mabomu ya Gongo la Mboto na Mbagala,” anasema Martha.
Lakini ilishauriwa pia Katiba ya Nchi ibadilishwe kulenga Mfumo wa Vyama vingi vya Siasa. Maana iliyopo ni ya Mfumo wa Chama kimoja. Kwa nini Katiba haibadilihshwi tokea mwaka huo tulipo anzisha Vyama vingi? Muda wote jibu muda hautoshi! Haki ni huleta Amani, maana Sheria zinazotungwa ni kulinda maslahi chama tawala. Rekebisha haya uone kama amani yetu inatoweka. Lakini sasa huwezi kuzungumza tu amani bila ya haki za msingi za Vyama na Raia wake. Mifano unayotoa kwa Nchi majirani kuwa na machafuko ni kwa sababu Viongozi hawazingatii Haki kwa wanaowaongoza, kwa maana hiyo Viongozi wetu wajifunze huko watekeleze yale ambayo Vyama na Wananchi wanayataka. Kigugumizi kinatoka wapi?