Waatalamu wa afya wataongezewa ujuzi -Nyembea

DAR ES SALAAM: TANZANIA na mataifa mengine 17 kutoka Afrika yanarajia kunufaika na mafunzo ya upasuaji wa mishipa ya damu kwenye ubongo yatakayodumu nchini kwa siku tano, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Hamad Nyembea anasema.
Akizungumza leo Mei 19, katika uzinduzi wa mafunzo maalumu ya upasuaji wa mishipa ya damu kwenye ubongo na magonjwa ya sakafu ya ubongo, Nyembea amesema mafunzo hayo yatashirikisha wataalamu wa shirikisho la wataalamu wa mifumo ya fahamu kutoka Ulaya.
Nyembea amesema mafunzo hayo yatakayotolewa katika hospitali zote kubwa nchini yanalenga kutoa huduma za kibobezi, hata hivyo yamekuja kipindi sahihi kwani wananchi wanaohitaji huduma ni wengi.
SOMA ZAIDI: Muhimbili uhaba wa damu ni 60% – HabariLeo
“Uvimbe, saratani, sakafu ya ubongo magonjwa haya yanazidi kuongezeka kwa hiyo mahitaji ni makubwa na serikali imekuwa ikiingia gharama kubwa kuwapeleka watu nje, lakini hata wananchi wenyewe wamekuwa wakiingia gharama kutibu magonjwa hayo,” amesema Nyembea.
Amesema lengo lingine la mafunzo hayo ni kujazia baadhi ya maeneo ambayo wataalamu wa huduma hizo walipelea. Amesema baadhi ya hospitali kubwa zina vifaa vya kisasa vinavyoweza kutoa huduma hizo.
SOMA ZAIDI: Familia 8 zaenda Muhimbili kupandikiza mimba
Ameongeza kuwa serikali imewekeza zaidi kwenye huduma za kibingwa na bobezi, hivyo wataalamu wa afya waliopo nchini watanufaika kwa kiasi kikubwa kupata ujuzi kuhusu huduma hizo.
“Tunataka hospitali zetu ziwe na uwezo mkubwa katika eneo hili na kwa kuanzia tumeita wenzetu kutoka Ulaya kuja kusaidia wataalamu wetu kupata mafunzo ili tuweze kuimarisha uwezo wa wataalamu,” amesema Nyembea.