Wachoshwa na mwekezaji, wataka umeme wa Tanesco

WANAKIJIJI wa Malangali Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro wameiomba serikali kuwapelekea huduma ya umeme wa Tanesco kutokana na wanaoutumia hivi sasa kutoka kwa mwekezaji Husk Power Systems Limited kushindwa kukidhi mahitaji yao.

Wakizungumza kwenye taftishi kuhusu maombi ya kurekebisha bei za umeme za wazalishaji wadogo iliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kilichofanyika kijijini hapo, walisema kuwa umeme wa mwekezaji umeshindwa kukidhi mahitaji na kwamba umekuwa ukikatika pindi hali ya hewa inapobadilika kutokana na kutegemea nguvu ya jua pekee.

Mkazi wa kijiji hicho, Said Salehe alisema kuwa mwekezaji huyo wakati anafika aliwahakikishia kuwepo kwa huduma hiyo ya nishati ya uhakika lakini hali ya sasa sivyo hivyo na anakwamisha maendeleo.

Salehe alisema kuwa mahitaji ya nishati yao ni makubwa kuliko huduma inayotolewa hivyo kuitaka serikali kuwapelekea huduma hiyo kupitia Tanesco.

Naye Katibu wa Baraza la ushauri la Watumiaji Huduma za Nishati na Maji (Ewura CCC), Goodluck Mmari alisema kuwa wananchi wanahitaji huduma na bei nzuri hivyo Ewura wanachunguza gharama za uwekezaji na maoni ya wananchi ili wapate bei halali ambayo haitamuumiza mwananchi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Michael Mshigwa alisema kuwa serikali imeelekeza kufanyia tathmini upya bei ambapo ilikuwa ni Sh 100 kwa uniti moja.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button