Wadau kuungana kukomesha udhalilishaji Zanzibar

TAASISI zinazotetea haki za wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na watoto Zanzibar zinatarajiwa kuungana kesho Jumamosi, Desemba 6, 2025, kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Udhalilishaji wa Kijinsia katika hafla maalum itakayofanyika katika Ofisi za TAMWA Zanzibar, Tunguu.
Hafla hiyo inalenga kuimarisha mshikamano wa wadau katika kupambana na ukatili wa kijinsia, hasa katika kipindi ambacho matukio ya ukatili yametajwa kuongezeka sambamba na matumizi ya teknolojia. Katika maadhimisho hayo, itawasilishwa ripoti maalum yenye maoni ya wadau kuhusu nafasi ya mwanamke katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mtazamo wa usawa wa kijinsia.
Ripoti hiyo itachambua ushiriki jumuishi na wenye usawa katika mfumo wa kisiasa, ikihusisha mafanikio, changamoto na mwenendo wa haki za wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika mazingira ya kisiasa na yale ya kidijitali.
Hafla hiyo inatarajiwa kukutanisha wadau wapatao 80 kutoka taasisi za kiserikali, zisizo za kiserikali pamoja na waandishi wa habari, kwa lengo la kuongeza uelewa na kuimarisha mbinu za pamoja za kukabiliana na udhalilishaji wa kijinsia.
Mjadala huo unatarajiwa kuweka mkazo katika athari za teknolojia na taarifa katika kusaidia au kuchochea ukatili wa kijinsia, hususan katika majukwaa ya mtandaoni. Taasisi zinazoratibu maadhimisho hayo ni pamoja na JUWAUZA, ZLSC, PYI, ZAFELA, PEGAO, ZAFAYCO, ZYF, THRDC pamoja na TAMWA Zanzibar.
Msingi wa kazi zao unachagizwa na mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo Tanzania, ikiwemo Zanzibar, imeridhia kama CEDAW, Itifaki ya Maputo, Azimio la Beijing (1995), na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan Lengo namba tano linalolenga usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
Kwa mwaka 2025, ujumbe wa kimataifa unaelekeza “TUUNGANE Kukomesha Ukatili wa Kidijitali Dhidi ya Wanawake na Wasichana,” huku ujumbe wa kitaifa ukisisitiza “Mitandao Salama ni Haki: Maliza Ukatili wa Kimtandao kwa Wanawake na Watoto.” SOMA: ‘Hapana tena ukatili wa kijinsia’
Kaulimbiu hizo zinahimiza matumizi salama ya teknolojia, uimarishaji wa mifumo ya udhibiti na kuripoti ukatili wa mtandaoni, pamoja na kulinda haki za wanawake na wasichana katika maeneo ya kidijitali. Kampeni ya Siku 16, iliyoanzishwa mwaka 1991, inaendelea kuwa jukwaa muhimu la kupaza sauti dhidi ya ukatili wa kimwili, kijinsia, kiuchumi, kisaikolojia na sasa ukatili wa kidijitali unaoendelea kuongezeka duniani.



