Wadau wa madini wateta mkutano wa jiolojia Dar

DAR ES SALAAM: WADAU mbalimbali wa sekta ya madini kutoka ndani na nje ya Afrika wamekutana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kimataifa wa PanAfGeo+ kujadili njia bora za kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za madini.
Mkutano huo umehusisha wataalamu wa jiolojia, wawakilishi wa serikali, na mashirika ya kikanda na kimataifa kama EuroGeo Surveys (EGS), Shirika la Jiolojia za Afrika (OAGS), na BRGM ya Ufaransa, kwa lengo la kubadilishana maarifa, kuimarisha ushirikiano, na kukuza uwezo wa kitaalamu barani Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 24, 2025, kwa niaba ya Waziri wa Madini Anthony Mavunde, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, amesema kuwa Serikali ya Tanzania imenufaika kwa kiasi kikubwa na mkutano huo ambao umeimarisha ushirikiano wa kimataifa na kusaidia kukuza uwezo wa kitaalamu ndani ya nchi.
Amebainisha kuwa mkutano huo umefungua fursa mpya za ushirikiano, mafunzo na uboreshaji wa usimamizi wa rasilimali kwa njia endelevu, hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Rais wa Shirika la Taasisi ya Jiolojia za Afrika, Dk. Rokhaya Samba, amesema kuwa awamu mpya ya mradi wa PanAfGeo+ inayotarajiwa kutekelezwa kati ya 2025 hadi 2029 inalenga kukuza maarifa kuhusu rasilimali za madini na uwezo wa kitaalamu katika nchi wanachama, huku akisisitiza umuhimu wa upimaji wa ramani kwa ajili ya kusaidia serikali kutambua rasilimali zilizopo na kufanya maamuzi sahihi katika majadiliano na wawekezaji.
“Mageuzi mapya katika teknolojia za kisasa, zana za ramani na mawasiliano yataanzishwa kupitia awamu hii ya mradi. Hii itaiwezesha Taasisi ya Jiolojia ya Afrika kuwa msaada mkubwa kwa serikali katika kupanga na kutekeleza sera bora za madini,” amesema Dk. Samba.
Naye Mratibu wa PanAfGeo+ kutoka Shirika la Jiolojia la Ufaransa, Jean-Claude Guilleneau, amefafanua kuwa mradi huo unaendeleza ushirikiano kati ya mashirika ya jiolojia ya Afrika na Ulaya.

Alisema hadi sasa, zaidi ya wataalamu 1,750 kutoka nchi 54 za Afrika wamenufaika na mafunzo ya kitaalamu yanayotolewa kwa lugha ya Kiingereza, Kifaransa, na Kireno, jambo linalosaidia kuongeza ufanisi na kuwafikia wadau wengi zaidi.
Guilleneau ameongeza kuwa mradi huo pia unazingatia uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa rasilimali muhimu, na kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi saba zinazopatiwa kipaumbele maalum kupitia mpango wa “madirisha ya nchi”, ukizingatia nafasi yake katika maendeleo ya sekta ya madini Afrika Mashariki.
Kupitia mkutano huo, nchi kama Rwanda, Uganda, Zambia, na Tanzania zimewasilisha miradi mipya ya ushirikiano katika sekta ya jiolojia, huku wataalamu wakijadili kwa kina mbinu za kuongeza ujuzi, kuboresha usimamizi wa rasilimali, na mchango wa sekta ya madini katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi barani Afrika.
Mradi wa PanAfGeo ulianzishwa mwaka 2016 kwa ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya na unafadhiliwa kwa sehemu na Tume ya Ulaya. Lengo kuu ni kuimarisha uwezo wa wataalamu wa jiolojia wa Kiafrika ili kuchangia maendeleo endelevu kupitia matumizi bora ya rasilimali za kijiolojia.