Wadau wasifia bajeti kugusa wananchi

DODOMA – BAJETI ya Serikali ya mwaka 2024/2025 imewavutia wadau wengi ambao wamesifi a mambo mbalimbali yaliyoainishwa kwenye bajeti hiyo.

Iliwasilishwa jana bungeni, Dodoma na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba. Mkuu wa Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino, Mwanza, Dk Isaack Safari alimpongeza Dk Mwigulu kwa namna alivyowasilisha bajeti kitaalamu na kusema imeakisi maneno, fikra na mwelekeo wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Alisema ameona mambo matatu muhimu yaliyomgusa na yaliyomgusa Mtanzania moja kwa moja.

“Kwanza ni juu ya Tanzania kwenye kilimo kama mambo yataenda vizuri halafu ikafuatiwa na elimu ya hali ya juu kwa kila mkulima kule kijijini, natumaini pakiwepo na uwezeshaji tutakwenda mbali katika kilimo, ningetamani hiyo iendane na elimu na ukaribu kwa mkulima kwa maana ya maofisa ugani,” alisema.

Alisema jambo jingine ni juhudi za wazi zilizoonekana za kutaka kupunguza gharama za usafiri wa daladala ambazo zitasaidia wafanyabiashara wadogo kutanua wigo wa biashara zao.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Msichana Initiative, Rebeca Gyumi amesifu kuondoa ushuru kwenye malighafi za kutengeneza taulo za kike na watoto kwani utasaidia kuelekea kwenye kupunguza bei za taulo hizo kwa Watanzania wa hali ya chini. “Naona ni hatua kubwa ya kupongezwa.

Lakini niseme kwamba hii ni hatua moja, ziko nyingine za kuchukua, kuna mlolongo wa kodi katika taasisi nyingine kama TMDA lakini pia kuondoa VAT itasaidia kupunguza bei,” alisema.

Mhadhiri wa Uchumi Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino, Damas Mushi alisema: “Kuna mapendekezo ya kupunguza kodi kwa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi na kuongeza kwa zinazotoka nje, hii inaonesha uzalendo dhidi ya viwanda vya ndani, itasaidia kukuza mitaji yao na kushindana na viwanda vya nje”.

Mkazi wa Mikocheni, Noel Moddy amesema bajeti hiyo imekaa kizalendo kwani imelenga kugusa nafasi ya kila Mtanzania. Mkazi wa Sengerema mkoani Mwanza, Laurent Moshi alisema kupitia mapendekezo yaliyotolewa na kama yatasimamiwa kikamilifu yataongeza pato la taifa.

Wabunge wasifu bajeti

Katika hatua nyingine, wabunge wamefurahishwa na bajeti hiyo huku wakipongeza fedha zilizotengwa kutekeleza miradi inayokwenda kuboresha maisha ya wananchi.

Pia wamepongeza hatua ya serikali ya kuongeza kikokotoo kwa wastaafu kutoka asilimia 33 hadi asilimia 40 na kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa malipo ya mkupuo.

Akitoa maoni, Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), alisema bajeti imegusa maeneo mengi ambayo yanagusa wananchi kwani fedha zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi iliyokwama na kukamilisha miradi ya kimkakati.

“Ni bajeti inayopunguza mambo ya kodi ambayo wabunge tulikuwa tukiyapigia kelele na mambo ambayo yanakwenda kukuza viwanda vya ndani ili tuondokane na utegemezi wa bidhaa za nje,” alisema.

Naye Mbunge wa Momba, Condester Sichalwe (CCM) alipongeza bajeti kwa sababu inakwenda kugusa maisha ya wananchi hususani katika utekelezaji miradi ya maji.

Pia alisema kumekuwapo na ongezeko la bajeti ya kilimo na kutokana na kuwa mwanamke ni mshiriki mkubwa katika sekta hiyo basi akizalisha zaidi uchumi wake utakua na kumfanya mwanamke kuwa na maamuzi. Mbunge wa Mlimba, Godwin Kunambi (CCM) alipongeza bajeti hiyo na kusema inakwenda kufungua uchumi wa wakulima na wafanyabiashara wa Mlimba kwa kujenga barabara yenye kilometa 62 kutoka IfakaraMbingu na Mbingu kwenda Chita JKT.

SOMA: Kitila abainisha uthabiti kiuchumi, kifedha

Naye Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alisema kupitia bajeti hiyo, Watanzania wameona nia njema ya serikali kutekeleza miradi ya miundombinu lakini pia imejikita katika sekta za uzalishaji kuinua maisha ya Mtanzania mmojammoja kuondokana na umasikini.

Kwa upande wa Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu (CCM) alisema bajeti hiyo ni ya wananchi kwa kuwa kimsingi imeangazia kuongeza uchumi na kilimo.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (Chadema) alisema anaamini mifuko ya hifadhi ya jamii ingekuwa na uwezo wa kulipa hadi asilimia 60 katika mafao ya mkupuo.

“Kikubwa nipongeze kwa hiyo hatua ya asilimia lakini kiukweli bado kwa sababu kabla ya sheria kubadilishwa ilikuwa ni asilimia 50 na habari njema ni kuwa angalau imefikia asilimia 40 na wamesema kuwa wataongezea kwa kipindi cha muda mfupi hadi watakapoona kuwa iko stable,” alisema.

Naye Mbunge wa Nkenge, Florent Kyombo (CCM) alisema hatua ya Rais Samia kuongeza kikokotoo kutapunguza makali waliyokuwa nayo wastaafu.

Habari Zifananazo

Back to top button