KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Mwenda amekutana na kuzungumza na wafanyabiashara mbalimbali wa Mkoa wa Mtwara na kuahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili wanapotekeleza majukumu yao hayo.
Akizungumza wakati wa kikoa hicho kilichofanyika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani humo, Kamishna huyo amesema ili wafanyabiashara hao waendelee kuwepo kwenye biashara wanapaswa kutatuliwa changamoto walizonazo.
Lengo la kikao ni kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabishara hao ili serikali iweze kushughulikia changamoto hizo jambo litalosaidia biashara zao kustawi na kuendelea kuongezeka katika mkoa huo kwa manufaa ya familia zao, mkoa na taifa.
SOMA: TRA Mtwara yavuka malengo ukusanyaji mapato
Amesema angependa kuona mkoa huo unaendelea kuongeza biashara na sio kupunguza biashara na ili ziongezeke ni lazima kuwe na ushirikiano baina yao na wafanyabiashra.
‘’Sisi tuna hela kwenu, nyie kila mnapofanya biashara kuna asilimia ambayo ni ya serikali hivyo kama Tra tutafanya kila tunaloweza kushirikiana, kurahisisha biashara ili ziendelee kuwepo,’’amesema Mwenda.
Aidha amewaahidi wafanyabiashara hao kuwa atazifanyia kazi changamoto zote walizozieleza kuwa zimekuwa kikwazo katika biashara zao hususani kukithiri kwa kodi na kuwapongeza namna wanavyolipa kodi.
Zakia Hakimu anayejishughulisha na shughuli ya ushonaji katika Mananispaa ya Mtwara Mikindani mkoani humo amesema: ‘’Ujio wa kamishna mkuu tuna imani kubwa kuna vitu vilivyokuwa vinaumiza vichwa vitakaa sawa hasa swala la kodi, utitiri wa kodi umekuwa mwingi sana tunazidi kuiomba serikali ituangalie katika hili.”
SOMA: TRA kuwaongezea faida wafanyabiashara
Mwenyekiti wa Soko la Samaki la Feri kwenye manispaa hiyo, Mwinyi Mzaina amese,a: ‘’Kulikuwa na changamoto mbalimbali katika biashara zetu zilizokuwa zinakwamisha mzunguko wa biashara hapa mtwara lakini tunashukuru tumeziahinisha kwa kamishna wamezichukua na kwenda kuzifanyia kazi.”