Wafanyabiashara wahimizwa kutumia bandari Tanzania

ZAMBIA: Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Luteni Jenerali Mathew Mkingule, amewahimiza wadau na watumiaji wa bandari kuendelea kutumia bandari za Tanzania kama lango kuu la biashara kwa nchi za Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Akizungumza jijini Lusaka jana Oktoba 15, 2025 wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Wadau na Watumiaji wa Bandari za Tanzania, Balozi Mkingule amesema Tanzania ipo tayari kutoa huduma bora, za kisasa na zenye ushindani mkubwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine za nchi hiyo.

Takwimu zinaonesha ongezeko la shehena ya mizigo kutoka na kuingia Zambia kupitia bandari za Tanzania kwa zaidi ya asilimia 55, kutoka tani milioni 2.2 mwaka 2023/24 hadi tani milioni 3.5 mwaka 2024/25, hali inayoashiria ufanisi mkubwa wa huduma zinazotolewa.

Ziara hiyo ya kimasoko nchini Zambia ni sehemu ya juhudi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na DP World Dar es Salaam na TEAGTL katika kuimarisha uhusiano wa kibiashara wa kikanda na kuendeleza diplomasia ya kiuchumi.




