Wagonjwa 1000+ kutoka nje watibiwa hospitali ya Kaloleni

ARUSHA: HOSPITALI ya Karoleni jijini Arusha imeendelea kuonyesha mafanikio makubwa katika sekta ya afya na kuibuka kuwa miongoni mwa vituo vinavyochangia ukuaji wa utalii wa afya nchini Tanzania, baada ya kuhudumia wagonjwa wageni zaidi ya 1,110 kutoka nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa leo Juni 6,2026 Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Maoinduzi (CCM)Taifa, Kenani Kihongosi alipitembelea na kukagua utendaji katika hospitali hiyo.
Kihongosi amesema serikali imewezesha upatikanaji wa zaidi ya Sh bilioni 2.2 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba, pamoja na zaidi ya Sh bilioni moja zilizotengwa kwa ajili ya maboresho ya hospitali hiyo, hatua inayolenga kuboresha huduma za afya karibu na wananchi.
“Kuwepo kwa huduma za kisasa kumefanya wagonjwa wasihitaji kusafiri mbali. Hii ni hatua kubwa ya kupunguza gharama na muda, lakini pia kuifanya Arusha kuwa kituo muhimu cha huduma za afya,” amesema.

Ameongeza kuwa upatikanaji wa huduma za kibingwa katika hospitali za mikoa na wilaya umepunguza kwa kiasi kikubwa rufaa za wagonjwa kwenda hospitali kubwa za rufaa, na hivyo kuboresha mfumo wa utoaji huduma nchini.
Amesema huduma hizo zimechangia kuongeza idadi ya wagonjwa hususani wanaotoka nje ya nchi, ambapo zaidi ya wageni 1,110 tayari wamepata matibabu katika hospitali hiyo, hatua inayoonesha kuimarika kwa nafasi ya Tanzania katika utalii wa afya.
“Tumefarijika kuona sasa kwamba mnaanza kufanya hiyo hospitali mnaita ya mashuhuri, sasa hivi lugha ya kawaida mashuhuri ni kama umaalumu fulani, lakini tumeona kwenye taarifa pia mpaka sasa zaidi ya watalii 1,110 wamepata huduma hapa,” amesema Kihongosi.

Aidha, amewataka watumishi wa sekta ya afya kuendelea kutoa huduma kwa weledi, upendo na uadilifu kutokuleta chuki katika sehemu za kazi, akisisitiza kuwa sekta ya afya inahitaji kujituma kwa kuwa inahusiana moja kwa moja na uhai wa binadamu.
Akitoa taarifa ya mradi huo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Arusha (DMO), Maduhu Nindwa amesema katika kipindi cha utekelezaji wa maboresho ya Hospitali ya Kaloleni, Serikali imetoa na kuwekeza jumla ya takribani Sh bilioni 2.25) kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.

Aidha, amesema hospitali imetumia zaidi ya Sh bilioni 758 kwa ununuzi wa dawa na vifaa tiba katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026.
Pia hospitali hiyi ospitali inatoa huduma za kibingwa na kibobezi zikiwemo huduma za Sikio, Pua na Koo, Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Magonjwa ya Ndani, huduma za macho , upasuaji wa jumla, Upasuaji wa Mifupa na huduma za Mionzi.
Pia huduma za Endoscopy na Colonoscopy, Mammography kwa uchunguzi wa saratani ya matiti, Maabara na vipimo vya kisasa, huduma za dharura, tiba mazoezi pamoja na huduma za usingizi na ganzi ,zote zikitolewa kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za afya bora na za kisasa kwa wananchi.

Pia ilielezwa kuwa kutokana na maboresho hayo, idadi ya wagonjwa imeongezeka kutoka wastani wa 151 hadi zaidi ya wagonjwa 450–501 kwa siku, na hospitali pia imeanza kuhudumia wagonjwa wa utalii wa afya kutoka ndani na nje ya nchi.



