Wakandarasi walipwa bil 254/-

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema ndani ya miezi miwili, serikali imetoa takribani Sh bilioni 254 kwa ajili ya kulipa wakandarasi wa ndani na nje wanaotekeleza miradi ya ujenzi.

Ulega amesema hayo jijini Dodoma wakati wa kukagua ujenzi wa barabara ya Ntyuka hadi Kikombo yenye urefu wa kilometa 76.

Advertisement

Amesema maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia ni kuhakikisha kazi zote za sekta ya ujenzi zilizokuwa imesimama zinaendelea kama zilivyopangwa.

“Na ndio maana utaona katika muda wa hii miezi mwili tumepata malipo ya wakandarasi ya takribani Shilingi
bilioni 254 ambazo wakandarasi wa ndani na nje wamelipwa fedha nyingi kwa matumaini ya kuoana kazi zikiendelea,”alisema.

Ulega aliahidi kukutana na wataalamu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na timu ya mkandarasi CHICO inayojenga kipande cha kilometa 8.2 katika barabara ya Ntyuka hadi Kikombo ili kujadili na kukubaliana namna ya kujenga barabara hiyo baada ya kulipwa madai yao.

Kampuni ya Chico inayojenga kilometa 8.2 ya barabara hiyo inadai takribani Sh bilioni 6.4.

“Nimemhakikishia serikali italipa madai yake ili kuendelea na kazi, na tumekubaliana kwenda kukaa na mkandarasi
na mimi na timu yangu ili tuzungumzie hili,” alisema.

Ulega alisema mwishoni mwa Februari mwaka huu serikali inatarajia kutoa fedha zingine za kutekeleza miradi ya miundombinu katika sekta ya ujenzi na kuiagiza Tanroads kuipa kipaumbele barabara hiyo ili ianze kujengwa haraka.

Kuhusu madai ya fidia, Ulega alisema katika siku za hivi karibuni tayari serikali imelipa fidia ya Sh bilioni 20 kwa wananchi ambao wamepisha miradi ya ujenzi katika maendeleo mbalimbali nchini na kuwahakikishia wananchi wa Ntyuka watalipwa fidia zao pindi taratibu zitakapokamilika.

Mbunge wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alisema baadhi ya wananchi walioguswa na
mradi huo wanadai faida ya Sh bilioni 7.4 na kuwa anatamani wananchi hao walipwe fidia zao.

Alisema kujengwa kwa barabara Ntyuka-Kikombo itamsaidia kupunguza gharama za usafiri kwa wananchi.

“Wananchi wanaoishi Ntyuka na wale wanaokuja Hospitali ya DCMC wamekuwa wakilipa nauli kubwa wakati mjini si mbali. “Hofu yangu kubwa, serikali itaingia gharama kubwa kwa sababu baadhi ya watu wakikuta changamoto
kwenye barabara za mchepuko wanatumia barabara zilizoanza kujengwa, hivyo kufanya uharibifu mkubwa.”

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri ameiomba wizara kuangalia namna ya kutumia fedha za
uwajibikaji kwa jamii kutoka kwa mkandarasi anayejenga barabara ya Ntyuka hadi Kikombo kutumika kuziimarisha baadhi ya barabara za Kata ya Kilimani ambazo haziko kwenye hali nzuri.

Aliomba baada ya mkandarasi kulipwa, kipaumbele kielekezwe katika kipande cha kilometa 8.2 ambacho kina kivuko cha reli ya kisasa ya SGR, kurahisisha usafiri na wananchi zaidi ya 200 watapata ajira.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *