Wakili Madeleka autaka ubunge Kivule

DAR ES SALAAM: MWANACHAMA wa ACT Wazalendo, Wakili Peter Madeleka, amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama chake kugombea ubunge wa Jimbo la Kivule, Dar es Salaam leo.
Hafla ya kuchukua fomu hiyo imefanyika katika ofisi za chama hicho na kuhudhuriwa na wanachama pia viongozi mbalimbali wa chama ngazi ya jimbo.

Fomu hiyo imekabidhiwa kwa Wakili Madeleka na Kaimu Katibu wa Jimbo la Kivule, Emmanuel Magoto.
SOMA ZAIDI
Akizungumza baada ya kupokea fomu, Madeleka ameeleza dhamira yake ya kuwatumikia wananchi wa Kivule kwa uadilifu na kuwahakikishia kwamba sauti zao zitasikika bungeni.

Amegusia changamoto nyingi zinazolikabili jimbo hilo, zikiwemo miundombinu mibovu ya barabara ambazo hazipitiki kwa mwaka mzima na hivyo kusababisha usumbufu kwa wakazi na kudhoofisha shughuli za kiuchumi.
“Wananchi wa Kivule na Watanzania kwa ujumla wamechoka na hali ngumu ya maisha. Bei za bidhaa zimepanda, ajira hakuna, huduma za afya na elimu bado ni changamoto,” amesema Madeleka.
Aidha, amezungumzia hali ya kisiasa nchini na changamoto za demokrasia, akisisitiza kuwa licha ya mazingira magumu, ni muhimu kwa Watanzania kushiriki katika mchakato wa uchaguzi kama njia ya kupigania mabadiliko.



