Wakurugenzi wasimamie maji yapatikane shule zote

KATIKA gazeti hili leo ipo habari kuhusu maelekezo ya Ofi si ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa wakurugenzi wa halmashauri kuhusu upatikanaji wa huduma za maji katika shule zote nchini.

Naibu Waziri, Zainabu Katimba alitoa maelekezo hayo akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mwantum Zodo (CCM) jana bungeni.

Mbunge huyo alitaka kujua sababu za serikali kutotumia magari ya kuchimba visima yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika halmashauri mbalimbali ili kumaliza changamoto ya maji katika shule za msingi na sekondari.

Advertisement

Tunaunga mkono rai ya Ofisi ya Rais, Tamisemi huku tukihimiza wakurugenzi kusimama kidete maji yapatikane katika shule zote nchini.

Tunasisitiza hili kwa kuzingatia ukweli kwamba, zipo shule nyingine, zikiwamo za mjini zisizokuwa na huduma ya uhakika ya maji.

Matokeo yake, katika baadhi ya shule, huwalazimu wanafunzi kuagizwa waende na maji kwenye vidumu kwa ajili ya matumizi yao binafsi na mazingira ya shule.

Huu ni usumbufu mkubwa kwa watoto. Maji ni muhimu kwa usafi binafsi wa wanafunzi, walimu na watumishi wengine. Kutokuwapo maji ya uhakika ni kikwazo kwa mazingira ya kujifunzia hasa kwa watoto wa kike.

Zipo ripoti ambazo zimekuwa zikionesha watoto wa kike wanavyopata shida wakati wa hedhi kutokana na ukosefu wa maji ya kutosha.

Ukosefu wa huduma ya maji ni miongoni mwa visababishi vya wanafunzi wa kike kukosa masomo wawapo kwenye hedhi na hivyo kuathiri maendeleo yao na elimu kwa ujumla.

Maji pia huboresha afya na usafi wa wanafunzi kwa maana ya kunywa, kuosha mikono na kufanya usafi wa mazingira na mwili.

Vilevile yanasaidia kupunguza magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu na mengine yanayoathiri utendaji wa wanafunzi shuleni.

Kwa kuzingatia umuhimu wa maji shuleni, tunahimiza agizo hili lisiishie kutolewa bungeni bali lifikishwe kwa
utaratibu rasmi kwa wakurugenzi wafanye utekelezaji hasa shule zisizokuwa na mfumo wa huduma hiyo.

Wakurugenzi hawana budi kufanya kazi bega kwa bega na wadau kuhakikisha yanapatikana maji ya kutosha, safi na salama kwa matumizi shuleni.

Ni wajibu wa viongozi hao wa halmashauri kusimamia na kuratibu miradi inayohusisha upatikanaji wa maji, ili
kuhakikisha watoto wote wanapata fursa sawa katika elimu.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *