Waliozusha mwanafunzi kupigwa Mwanza wasakwa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa.

JESHI la Polisi mkoani Mwanza linawasaka wananchi waliozusha taarifa za kupigwa hadi kufariki mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Mlimani, Kata ya Bugarika, wilayani Nyamagana, Leonia Amiri (16).

Taarifa hizo zilizotolewa Julai 11,2024 zilidai mwanafunzi huyo alipigwa na Mwalimu hadi kumsababishia umati, hatua iliyopelekea wananchi kukusanyika shuleni hapo kwa fujo, akiwemo mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Christina Joshua (35) ambaye tayari anashikiliwa na Jeshi la polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC), Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa ametembelea Kata hiyo kuwapatia wananchi elimu ya ulinzi na usalama, akawataka kuifanyia uchunguzi wa kina taarifa yoyote wanayopokea, badala ya kufanya uzushi unaoweza kupelekea uvunjifu wa amani.

Advertisement

Soma:Polisi yadaka wezi wa magari, bajaji

“Hii ilikua ni hatari kwa walimu wa shule hiyo kama jeshi la polisi lisingewahi eneo la tukio kudhibiti uvunjifu wa amani, ambao ungeleta maafa kwa watu na mali.

“Tunawasaka wote waliosababisha taharuki. Uchunguzi unaonesha mama mzazi wa mwanafunzi alipokea taarifa za uzushi kwamba kuna mwanafunzi amepigwa hadi kuzimia na wengine wakisema amefariki,” amesema RPC na kufafanua zaidi kwamba:

Uchunguzi unaonesha mama huyo ana watoto wawili, mmoja anasoma shule ya msingi na wa pili sekondari. Huyo wa sekondari ana changamoto kidogo ya kiafya, hivyo baada ya kusikia kuna mtoto amepigwa hadi kuzimia, akadai kwa vyovyote ni wa kwake kutoka na udhaifu alionao, kisha akakusanyana na wananchi wengine kuvamia shule.

Jeshi la Polisi limekuwa likionya kuhusu tabia ya kutoa taarifa zisizo sahihi zinazoweza kusababisha uvunjifu amani.