BODI ya Maziwa imetoa elimu pamoja na maziwa kwa watoto wenye mahitaji maalumu kutoka shule mbalimbali zilizopo Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.
Elimu hiyo imetolewa leo Septemba 23,2024 wakati wa uzinduzi wa unywaji maziwa shuleni uliofanyika katika manispaa hiyo na miongoni mwa shule zilizopatiwa maziwa pamoja na elimu hiyo ni Sekondari ya Mtwara Ufundi, Shule ya Msingi Shangani, Rahaleo na Mikindani.
Akizungumza na HabariLeo, Ofisa Masoko wa Bodi ya Maziwa , Hamisi Kilimbi amesema lengo la serikali ni kuhamasisha jamii kujua umuhimu wa unywaji wa maziwa.
“Takwimu za mwaka 2024 zinaonesha kuwa nchi ya Tanzania iko nyuma sana kwenye unywaji wa maziwa ambapo kila mtanzania anakunywa lita ya maziwa 67.5 kwa mwaka na kwa mujibu wa mashirika ya chakula duniani yanapendekeza kila mtanzania anatakiwa kunywa angalau lita 200 ya maziwa kwa mwaka,” Kilimbi amesema
SOMA: DC Mbogwe atoa elimu ya lishe
Hata hivyo kutokana na kutoridhisha kwa takwimu hizo, bodi hiyo imetengeneza program mbalimbali za kuhamasisha unywaji wa maziwa ambapo miongoni mwa program hizo ikiwemo unywaji maziwa mashuleni.
Program hiyo ina lengo la kumjengea mtoto tabia ya kunywa maziwa toka akiwa mtoto hadi anapokuwa pia mazoea ya kuweza kuipeleka elimu hiyo hadi kwa vizazi na vizazi.
SOMA: Lishe duni sababu wanafunzi kuchukia hisabati
Msajili kutoka Bodi ya Maziwa , Deorinidei Mng’ong’o amesema dhumuni la tukio hilo la unywaji wa maziwa ambalo maadhimisho yake hufanyika kila ifikapo Septemba 25 ya kila mwaka ni kuhamasisha unywaji wa maziwa mashuleni na kuwafundisha watoto umuhimu wa unywaji maziwa kwani yanafaida nyingi ikiwemo kuupa mwili afya.
Ametoa rai kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika tukio hilo ambalo litafanyika shule ya msingi misufini kwenye manispaa hiyo.
Kwa upande wake daktari wa mifugo kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Subira Sendei amesema hali ya unywaji wa maziwa kwa mkoa huo sio kubwa kutokana na mifugo ya ng’ombe kuwa michache.
Aidha mkoa huo una jumla ya ng’ombe 48,000 hivyo hutegemea maziwa kutoka nje ya mkoa huku akiishukuru bodi hiyo kwa kuja kufanya kongamano katika mkoani humo kwani kutawafanya wananchi kujifunza na kuingia kwenye ufugaji ulio bora.
Mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari ya Mtwara Ufundi kwenye manisapaa hiyo moja ya shule zilizopatiwa maziwa na elimu hiyo, Amos Claver “Naishukuru serikali kwa kuwa na jambo hili zuri ambalo lina lengo la kuhamasisha ufaulu wa mwanafunzi,afya na ukuaji bora,”amesema.